Madrid, Hispania
Rais wa miaka mingi wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez ameibuka mshindi katika uchaguzi wa nafasi hiyo na hivyo kupata ridhaa ya kuendelea kuongoza kwa miaka mingine minne.
Uchaguzi wa safari hii ambao uliandamana kampeni za hapa na pale zilizotawaliwa na mizengwe dhidi ya Perez ulifanyika Jumapili Juni 7, 2026 lakini Perez mzee mwenye umri wa miaka 79 alimshinda Enrique Riquelme kijana wa miaka 37.
Huu unatajwa kuwa ni uchaguzi wa kwanza katika kipindi cha miaka 20 ambao umeonekana kuwa na ushindani dhidi ya Perez ambaye hata hivyo ameweza kupata ushindi kwa asilimia 65 dhidi ya 35 za Riquelme.
Wanachama 33,555 wa Real Madrid walishiriki uchaguzi huo ukiwakumbusha ule wa mwaka 2006 ambao nao ulionesha kuwapo upinzani dhidi ya Perez tofauti na hivyo kwenye chaguzi nyingine imekuwa kama hakufanyiki uchaguzi.
Muda mchache kabla ya matokeo ya mwisho kutangazwa rasmi, Riquelme alikuwa wa kwanza kukiri kushindwa na kumpongeza Perez kwa ushindi ingawa aliweka wazi kuwa Real Madrid haiwezi kufikisha miaka mingine 20 bila ya uchaguzi.
Perez ndiye aliyechukua uamuzi wa kuitisha uchaguzi mapema licha ya kwamba bado alikuwa na kipindi kingine cha miaka miwili, uamuzi huo unatokana na mwenendo mbaya wa timu.
Real Madrid imeshindwa kubeba taji lolote la maana kwa misimu miwili huku mahasimu wao Barcelona wakifanikiwa kulitetea taji la La Liga katika msimu wa 2025-26 uliomalizika mwezi uliopita.
Akizungumzia ushindi wake, Perez alisema namba za kwenye uchaguzi huo ni ishara kubwa ya kura za kuwa na imani naye katika kuisimamia klabu hiyo.
Kimataifa Perez ashinda uchaguzi Real Madrid
Perez ashinda uchaguzi Real Madrid
Read also
