Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na wapo tayari kuikabili Bulgaria kesho Ijumaa.
Stars itatupa karata yake ya kwanza katika michuano ya Fifa Series 2024 katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Baku, Azerbaijan.
Morocco alisema mchezo huo ni kipimo kizuri kwa wachezaji wake ambao wengi wanaandaliwa kwa ajili ya kikosi cha baadaye na wametilia mkazo kuhakikisha wanapata ushindi.
Naye kipa wa Stars, Abutwalib Mshery amesema wamejiandaa vizuri na kwamba mchezo huo ni fursa kwao kwa sababu unaandaliwa kwa ajili ya timu ya baadaye itakayocheza Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2027) ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji pamoja na Kenya na Uganda.
Naye beki Novatus Miroshi alisema: “Kucheza na timu zinazotoka nje ya Afrika ni mara ya kwanza au chache, ila ni fursa kwa wachezaji wengi kwani itawajenga kuelekea mashindano ya kufuzu Afcon na ni kipimo kizuri kwetu. Benchi la ufundi watakuwa wameshajua tunatakiwa tufanye nini kizuri na kipi tunatakiwa kuongeza hivyo naamini utakuwa mchezo mzuri ambao utatujenga,”.
Baada ya mchezo huo nyota wa Stars wanaotoka klabu za Simba na Yanga watarejea nchini kuungana na timu zao ambazo zinajiandaa na mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kimataifa Morocco: Tuko tayari kuivaa Bulgaria
Morocco: Tuko tayari kuivaa Bulgaria
Read also