Paris, Ufaransa
Klabu ya Paris St-Germain (PSG) ya Ufaransa ina mpango wa kumpa mkataba mpya nyota wake Lionel Messi wakati huo huo Barcelona ikiwa katika mkakati wa kumsajili kwa mara nyingine.
Messi amekuwa na historia ya kipekee na Barcelona, klabu ambayo ilimkuza katika timu zake za watoto kabla ya kuwa staa wa timu kubwa na kushinda karibu kila kitu katika soka akiwa haijui klabu nyingine kubwa zaidi ya Barcelona lakini akaondoka mwaka 2017 na kujiunga na miamba hiyo ya Paris..
Wakati Barca na PSG zikilifanyia kazi suala hilo, Messi, mwenye umri wa miaka 35, kwa upande wake amesema kwamba hawezi kutangaza uamuzi wowote kuhusu wapi anataka kwenda hadi baada ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar, Novemba mwaka huu.
Habari za ndani zinadai kwamba Messi mwenyewe haoni tabu kurudi Barca na analifurahia jambo hilo hasa kwa kuwa hata kuondoka kwake Barca kulitokana na kanuni za matumizi ya fedha kuibana klabu hiyo na hivyo kujikuta ikimruhusu aondoke shingo upande.
Kurejea kwa Messi pia kunahusishwa na kauli ya hivi karibuni ya mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Jordi Cruyff ambaye alisema kwamba jiji la Barcelona limeanza kuwa moto baada ya mambo kuanza kuwa mazuri katika klabu hiyo akifafanua kwamba hali hiyo imechangiwa na hatua ya kusajili wachezaji ambao wamefuata ndoto zao badala ya fedha.
Messi naye anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanafurahia na kujivunia kuichezea Barca na hivyo kinachoonekana ni kwamba suala la kurudi katika klabu hiyo ni jambo linalosubiri muda tu.
Rais wa klabu ya Barcelona, Joan Laporta aliwahi kumzungumzia Messi akisema kwamba klabu yake haijafunga ukurasa kwa mchezaji huyo na wana jukumu la kuhakikisha anakuwa na mwisho mzuri akiwa Nou Camp.
Kauli ya Laporta ilifuatiwa na kauli ya kocha wa Barca, Xavi aliyewahi kuitaka klabu hiyo imsajili Messi mara baada ya mkataba wake na PSG kufikia ukomo. Mkataba wa Messi na PSG unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu.
Kimataifa Messi kurudi Barca ni suala la muda tu
Messi kurudi Barca ni suala la muda tu
Read also
