New York, Marekani
Bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, Deontay Wilder amerejea ulingoni kwa kishindo usiku wa kuamkia leo baada ya kumtwanga Robert Helenius katika raundi ya kwanza tu ya pambano lao lililofanyika Brooklyn, New York.
Wilder, bondia wa Marekani mwenye umri wa miaka 36 amerejea ulingoni kwa mara ya kwanza tangu amtwange Tyson Fury katika pambano lake la mwisho lililofanyika Oktoba mwaka jana.
Ngumi kali ya mkono wa kulia ya Wilder iliyompata kisawasawa usoni ndiyo iliyoonekana kumvuruga mpinzani wake huyo kutoka Finland ambaye kabla hajakaa sawa alijikuta akisukumiziwa ngumi nyingine kali ya mkono wa kushoto ambayo ilitosha kumfanya ‘alambe sakafu’.
“Huu ni usiku wa kipekee,” alisema Wilder baada ya ushindi huo wa mapema na kuongeza, “nilimvutia kasi, nilimfanya anisogelee, nilitaka niweze kumfikia kwa haraka, nilimuweka sawa akanifikia nami nikamfikia na kumshambulia.”
Ushindi huo unamfanya Wilder aboreshe rekodi yake ambayo sasa inaonyesha amepigana mara 43, mara 42 ameshinda kwa KO na mara moja ametoka sarea.
Baada ya ushindi huo, Wilder sasa anatarajia kuzipiga na Mmarekani mwenzake na bingwa wa zamani wa dunia, Andy Ruiz Jr au dhidi ya bondia wa Ukraine, Oleksandr Usyk ingawa pia katika siku za karibuni alinukuliwa akisema kwamba angependa kupanda ulingoni dhidi ya bondia wa Uingereza, Anthony Joshua kwa anachoamini kuwa hilo litakuwa pambano la ngumi namba moja duniani.
“Nani anafuata? Niko tayari kwa yeyote, Andy Ruiz, Usyk au mwingine yeyote, nimerudi ulingoni, burudani imerudi katika ‘kitengo’ cha ngumi za uzito wa juu,” alisema kwa kujigamba baada ya ushindi wake dhidi ya Helenius.
Ngumi Wilder amtwanga Helenius raundi ya kwanza
Wilder amtwanga Helenius raundi ya kwanza
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
