Na mwandishi wetu
Licha ya Simba kutoa tamko juu ya mchezaji wake, Dejan Georgijevic kuhusu kuvunja mkataba wake lakini imeeleza kuwa haikuwa ikiridhishwa na kiwango cha mshambuliaji huyo.
Hayo yameelezwa baada ya jana, Dejan raia wa Serbia maarufu kwa jina la Mzungu kueleza kuvunja mkataba wake wa miaka mitatu na Simba kutokana na kukiukwa kwa mambo ya msingi ndani ya mkataba wake.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema hata wao hawajabaini hasa kilichomvuruga mchezaji huyo na kama kulikuwa na mambo ya kuzungumza wangezungumza lakini inaonekana ameamua kufanya alichokitaka.
Alisema kuwa pamoja ya kwamba ni mchezaji mzuri lakini ameshindwa kuwaonyesha kile ambacho Wanasimba walikuwa wakikitarajia kutoka kwake, ndiyo maana walimpa mkataba mrefu kuliko mchezaji mwingine.
“Ni kweli Mzungu ana balaa, ana hatari lakini ameshindwa kutuonyesha sisi Wanasimba kile ambacho tulikuwa tunakitaraji kutoka kwake, sasa hilo linabaki sio jambo letu, sisi tuliweka imani tulimpa mkataba tena wa muda zaidi kuliko mchezaji yeyote wa Simba, mkataba wa miaka mitatu.
“Kwa hiyo ni kwa sababu ya imani yetu kwake tuliamini angeweza kufanya mambo makubwa kutokana na uwezo wake lakini imekuwa tofauti na ameondoka mapema, niseme balaa la Mzungu limeisha rasmi,” alisema Ally.
Awali, kabla ya Dejan kuandika mitandaoni kuhusu kuvunja mkataba na Simba na kurejea Dar es Salaam, siku chache nyuma alionekana akizozana na Augustine Okrah wakati mechi yao dhidi ya Malindi ikiendelea kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ingawa haijafahamika hasa chanzo cha Dejan kuvunja mkataba lakini inajumuishwa na ugomvi huo, pia ikielezwa mchezaji huyo hakuridhishwa na nafasi finyu aliyokuwa akipewa kucheza tangu atue msimu huu.
Dejan aliyedumu Simba kwa siku 52 pekee, amecheza mechi sita kwa takriban dakika 312 na kufunga bao moja kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara waliyoshinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Mapema leo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Simba ilieleza kusikitishwa na kitendo cha Dejan kuvunja mkataba kupitia taarifa ya mitandaoni, ikisisitiza kuwa itachukua hatua stahiki juu ya kitendo hicho cha mchezaji huyo.
Soka Simba: Kiwango cha Mzungu hakijaturidhisha
Simba: Kiwango cha Mzungu hakijaturidhisha
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
