Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya Tabora United upo katika hatua za mwisho kuachana na kocha wao mkuu, Goran Kopunovic kutokana na mwenendo mbaya uliokuwa nayo timu hiyo kwenye Ligi Kuu NBC.
Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Thabiti Kandoro alisema wameshakutana na kocha huyo na kumueleza namna wasivyoridhishwa na mwenendo wa timu yao na wapo katika hatua za mwisho kusitisha mkataba wake.
“Bado hatujaachana naye sababu kuna haki zake tunasubiri kumkamilishia lakini kama uongozi tupo katika mchakato wa kumsaka mbadala wake atakayeiongoza timu yetu katika mechi zilizobaki,” alisema Kandoro.
Mtendaji huyo alisema matokeo ambayo timu yao inayapata hayaendani na ubora wa kikosi walichokisajili msimu huu ndio maana wanataka kuachana na Mserbia huyo.
Tabora inayoshiriki ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu huu inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi 21 na tayari imecheza idadi kama hiyo ya mechi na imebakiwa na mechi tisa kabla msimu kumalizika.