Na mwandishi wetu
Baada ya Simba kuchezea kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga, mkuu wa mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amewataka mashabiki wa Simba wasahau matokeo hayo kwani hayajabadili chochote kwenye historia ya vipigo baina ya timu hizo.
Makalla ambaye ni shabiki wa Wekundu hao aliyasema hayo akifafanua kufungwa huko hakujapindua historia yoyote ya vipigo walivyowahi kuichapa Yanga ikiwemo 5-0 na 6-0 hivyo wasiwe na wasiwasi na waendlee na kazi kama kawaida bila ya mawazo yoyote.
“Mi niwashauri kuwa habari za kufungwa wazisahau waendelee kuchapa kazi kama kawaida, sababu matokeo hayo hayajapindua historia yoyote maana Yanga ilishafungwa 6-0, 5-0, kwa hiyo wala wasipate taabu, iko hivyo,” alisema Makalla.
Kiongozi huyo amekumbushia vipigo hivyo vilivyotokea mwaka 1977 ambapo Simba ilishinda kwa kuichapa Yanga mabao 6-0 huku mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni akifunga mabao matatu (hat trick) peke yake.
Kipigo kingine ni kile cha mwaka 2012 ambapo Simba iliichapa Yanga mabao 5-0, vipigo ambavyo vinaonekana kuwa kama deni kwa Yanga.
Hata hivyo, mashabiki wa Yanga wamekuwa wakitamba kulipiza kisasi baada ya ushindi wao huo wa Jumapili iliyopita wa mabao 5-1 uliopatikana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
