London, England
Mtu mmoja anayeaminika kuwa shabiki wa Tottenham Hotspur, amekiri mahakamani kuwa alimpiga kipa wa Arsenal, Aaron Ramsdale wakati wa mechi ya Ligi Kuu England baina ya timu hizo.
Ramsdale alipigwa teke kwa nyuma katika mechi baina ya timu hizo mahasimu wa kihistoria wa jiji la London iliyochezwa Januari 15 na Arsenal iliyokuwa ugenini kuichapa Spurs mabao 2-0.
Shabiki huyo, Joseph Watts mwenye umri wa miaka 35 kutoka Dalston, alifika katika Mahakama ya Uxbridge leo Ijumaa na kukiri kumpiga kipa na kurusha sarafu nne uwanjani wakati wa mechi hiyo.
Ramsdale alikuwa mwiba kwa Spurs katika mechi ya mahasimu hao na mahakama ilielezwa kwamba alikuwa akishangilia ushindi lakini wakati anachukua vifaa vyake nyuma ya goli ndipo alipopigwa.
Inadaiwa kwamba shabiki huyo alishuka kutoka sehemu aliyokaa jukwaani, akaruka uzio na bango la matangazo kabla ya kumkaribia Ramsdale na kumpiga kisha akarudi jukwaani huku akikimbia.
“Sikuwahi kumshuhudia mtu hapo kabla akiingia uwanjani na kunipiga na sidhani kama jambo hilo linakubalika yaani nivamiwe na kupigwa nikiwa kazini,” alisema Ramsdale ambaye pia ni kipa wa timu ya Taifa ya England.
Aliongeza kwamba ana hofu tukio kama hilo linaweza kutokea siku zijazo wakati shabiki aliyefanya kosa hilo alikiri kwamba alikuwa amelewa.