Roma, Italia
Rais wa Shirikisho la Soka Italia (FIGC), Gabriele Gravina ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo ikiwa ni siku chache baada ya taifa hilo lenye heshima katika soka duniani kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Italia, mabingwa wa Kombe la Dunia 2006, wameshindwa kufuzu fainali hizo kwa mara ya tatu mfululizo kuanzia 2018 na 2022 na sasa watakosekana katika fainali za mwaka 2026 zitakazoanza rasmi Juni 11 katika nchi za Mexico, Canada na Marekani.
Uamuzi wa Gravina kujiuzulu nafasi hiyo umechangiwa na shinikizo kutoka kwa wanasiasa na wadau mbalimbali wa soka ambao wamechukizwa na kufeli kwa timu hiyo licha ya heshima ya muda mrefu ya Italia katika soka duniani.
Baada ya kiongozi hiyo, kujiuzulu, mwingine aliyechukua uamuzi huo ni kipa mkongwe, Gianluigi Buffon ambaye naye ametangaza kuacha kuichezea timu ya taifa huku ikiaminika kuwa kocha Gennaro Gattuso naye yuko mbioni kuchukua uamuzi huo.
Waziri wa Michezo wa Italia, Andrea Abodi ametaka yafanyike mabadiliko katika uongozi wa soka nchini humo hasa baada ya nchi hiyo kushuhudiwa ikikosa mara mbili kushiriki fainali hizo chini ya Gravina.
“Ni jambo lililo wazi kwa kila mtu kwamba uongozi wa soka Italia unahitaji kufumuliwa na utekelezaji wa jambo hilo unatakiwa kuanzia kwa uongozi wa FIGC,” alisema Abodi.
Matarajio ya Italia kufuzu fainali za Kombe la Dunia yalikwama kwenye mechi za play-off baada ya timu hiyo mabingwa mara nne ya Kombe la Dunia kushindwa katika mikwaju ya penalti mbele ya Bosnia & Herzegovina.
Gravina alichukua uongozi wa FIGC mwaka 2018 kutoka kwa Carlo Tavecchio ambaye pia alijiuzulu baada ya Italia au Azzurri kushindwa kufuzu fainali hizo.
