Na mwandishi wetu
Simba imeendelea kuifukuzia Yanga kileleni mwa Ligi Kuu NBC baada ya kuitandika Singida Big Stars mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
Jean Baleke ndiye aliyekuwa wa kwanza kuziona nyavu za Sngida Big katika dakika ya nane ya mchezo huo alipoandika bao la kwanza akiuwahi mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Clatous Chama.
Dakika 12 baadaye, Saido Ntibazonkiza aliziona nyavu kwa bao la kichwa akiunganisha mpira wa adhabu lakini Bruno Gomes akaibua matumaini kwa Singida Big alipofunga bao pekee la timu hiyo.
Bao la Gomez ambalo liliibua matumaini ya Singida kupata bao jingine, lilitokana na mpira wa adhabu ambao aliupiga mchezaji huyo kiufundi kwa guu lake la kushoto akiwa nje kidogo ya eneo la 18.
Gomez alimchungulia kipa wa Simba Aishi Manula na kupiga mpira ambao ulimshinda kipa huyo licha ya kujaribu kuufuata juu kwenye kona ya kushoto kwake lakini juhudi zake hazikuzaa matunda.
Kipindi cha pili kila timu ilionyesha uhai, Simba wakitaka kuongeza bao la tatu wakati Singida wakipambana kusawazisha na mwishowe walikuwa ni Simba waliopata bao dakika ya 63 lililofungwa na Pape Sakho.
Sakho alifunga bao hilo kwa shuti kali akiunganisha pasi ya juu aliyochomekewa na Shomari Kapombe ambaye alionyesha juhudi na kuuwahi mpira wa juu kabla ya kuunganisha pasi ya moja kwa moja iliyomkuta mfungaji.
Dakika ya 79, Baleke alishindwa kuipatia Simba bao la nne baada ya kuunganishiwa pasi ya chini chini na Mohammed Hussein lakini akiwa na kipa Haule wa Singida Big alipiga mpira wa chinichini ambao uliokolewa na kipa huyo.
Pamoja na juhudi walizozionyesha Singida Big lakini kadri muda ulivyozidi kuyoyoma walizidi kuishiwa nguvu na kuna wakati walijikuta wakiutafuta mpira ambao wachezaji wa Simba wakiongozwa na Chama katika eneo la kati walikuwa wakiuchezea mpira huo kwa raha zao.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa leo, Prisons ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani imeshindwa kuutumia vyema uwanja huo baada ya kuambulia sare ya 0-0 kwa Mtibwa Sugar.
Soka Simba yaipiga Singida Big
Simba yaipiga Singida Big
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
