London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekiri kuwa ukame wa kukosa kubeba taji kwa miaka sita limekuwa jambo gumu kwa timu hiyo kulikubali.
Arteta ametoa kauli hiyo wakati timu yake ikijiandaa kuumana na Man City, Jumapili Machi 22, 2026 katika mechi ya fainali ya Kombe la Carabao, mechi ambayo huenda ikawa sababu ya kuufuta ukame huo.
Kocha huyo ataingia uwanjani kukabiliana na bosi wake wa zamani, Pep Guardiola kwenye Uwanja wa Wembley, mechi ambayo pia itakuwa jaribio la kwanza kwa Arsenal katika kusaka mataji matatu kwa msimu mmoja.
Mara ya mwisho Arsenal kubeba taji ilikuwa mwaka 2020 walipobeba Kombe la FA katika msimu wa kwanza wa Arteta na timu hiyo.
Kwa mantiki hiyo mechi yao ya Jumapili na Man City ni mechi ya kwanza ya fainali tangu timu hiyo ifikie hatua kama hiyo mara ya mwisho miaka sita iliyopita.
Akizungumzia kuelekea mechi hiyo, Arteta alisema ni mechi iliyobeba hatma yao ingawa kilichopo ni kwamba shauku ya kubeba taji wamekuwa nayo kwa wakati wote na angependa wawe na shauku hiyo kwa kila mwaka.
“Ni dhahiri kwamba shauku ipo ya kushinda kila wakati na hilo halijabadilika kama nikishinda taji mara moja, mbili au hata mara tano, napata shida kukubali ukweli kwamba nahitaji kushinda kila mashindano ninayoshiriki,” alisema Arteta.
Alisema unapokuwa katika nafasi aliyopo na kupita miaka mingi bila kubeba taji ni wazi umuhimu wa kufanya hivyo unaongezeka na unazidi kushawishika kwa sababu ni wazi unakuwa mwenye kulihitaji jambo hilo na hiyo ndiyo hali inayowakabili wao kwa wakati huu.
Kocha huyo pia alikiri kwamba ni lazima kuukubali ukweli kwamba katika michezo kuna wakati wachezaji au timu nyingine inaweza kuwa bora kukushinda na hapo unachoweza kufanya ni kujiangalia na kufanya lolote linalowezekana na kuwa bora na hilo ndilo wanalolifanya.
