Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imetangaza rasmi kuachana na beki wa kati wa timu hiyo, Pascal Wawa baada ya kudumu naye kwa misimu minne kabla ya kuelezwa kuwa mkataba wake utafikia tamati mwishoni mwa mwezi huu.
Simba ilitoa taarifa hiyo leo kupitia akaunti za mitandao yao ya kijamii juu ya beki huyo ambaye ni miongoni wa wachezaji muhimu waliochangia mafanikio ya timu hiyo kwa misimu minne iliyopita.
“Baada ya kutumikia timu yetu kwa misimu minne, Pascal Wawa hatakuwa sehemu ya kikosi chetu cha msimu ujao,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza kuwa mchezo wa kesho wa Simba na Mtibwa utakuwa wa mwisho kwa bei huyo.
Wawa ambaye ni raia wa Ivory Coast alianza kuonekana Tanzania kwa mara ya kwanza akikipga klabu ya Azam alikodumu kwa miaka miwili kabla ya kutimkia Al-Merreikh ya Sudan msimu wa 2016-17.
Baadaye Wawa alirejea nchini na kujiunga na Simba msimu wa 2018/19 alikodumu mpaka sasa na kuisaidia Simba kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu, mawili ya FA, na kuisaidia timu hiyo kufika hatua ya robo fainali mara mbili kwenye michuano ya klabu Afrika.
Kuachwa kwa Wawa imekuwa mwendelezo wa kuiweka sawa timu hiyo kuelekea msimu ujao baada ya wiki iliyopita pia Wekundu hao kumuaga kiungo wao Mzambia, Rally Bwalya anayetarajiwa kwenda kujiunga na Amazulu ya Afrika Kusini.
Soka Wawa aachwa Simba
Wawa aachwa Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
