Na mwandishi wetu
Klabu ya JKT Queens imesema baada ya kutolewa hatua ya makundi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, sasa wanajipanga upya kivingine kuelekea msimu ujao.
Mwenyekiti wa JKT Queens, Esther Joseph alisema wamejifunza mambo mengi wanayohitaji kuyafanyia kazi ikiwemo kutengeneza kikosi bora chenye ushindani wa kwenda kuchukua Kombe la Afrika mwakani.
“Tumepokea matokeo tuliyoyapata tukiamini si mwisho wetu, tunaingia tena vitani kujipanga kurudi upya kwa ajili ya msimu ujao lakini pia kufanya vizuri kwa mara nyingine kwenye Ligi Kuu ya Wanawake,” alisema.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa JKT Queens, Esther Chabruma (pichani juu) alisema wakati wanakwenda kwenye mashindano hayo walitamani kufanya vizuri zaidi na kuchukua taji lakini mambo yamekwenda tofauti.
Alisema wanahitaji kujipanga zaidi kuanzia kwenye ligi ikiwezekana wapate nafasi nyingine ya uwakilishi wa kimataifa.