Na mwandishi wetu
Namungo imevuruga hesabu za Simba kuishusha Yanga kileleni na hatimaye kubeba taji la Ligi Kuu NBC baada ya kuilazimisha sare ya bao 1-1 matokeo ambayo yanakuwa faraja kwa Yanga.
Katika mechi baina ya timu hizo iliyopigwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa Lindi, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Jean Baleke katika dakika ya 27 kufuatia mpira wa faulo uliopigwa na Saido Ntibazonkiza.
Dakika sita kabla ya timu hizo kwenda mapumziko, Namungo walizima matarajio ya Simba kutoka na pointi zote tatu baada ya kusawazisha bao kupitia kwa Hassan Kabunda.
Kabunda alifunga bao hilo akiuwahi mpira ambao kipa wa Simba, Ally Salim alishindwa kuuokoa, mpira huo ulitokana na kona iliyochongwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Shiza Kichuya.
Simba hata hivyo katika mechi hiyo haikuwatumia wachezaji wake wengi tegemeo ambao wamezoeleka kuwamo katika kikosi cha kwanza isipokuwa Ntibazonkiza, Baleke na Joash Onyango ambao hawakuweza kuisaidia timu hiyo kupata ushindi.
Matokeo hayo sasa yanaiweka Simba pagumu katika mbio za kuivua Yanga taji la ligi kwani yanafifisha matumaini yaliyoibuka baada ya timu hiyo kuwachapa mahasimu wao Yanga mabao 2-0 hivi karibuni.
Ilitarajiwa kwamba baada ya ushindi wa mechi na Yanga, Simba ingeendelea kutoa vichapo huku ikiisubiri Yanga iteleze japo kwenye mechi moja pamoja na sare moja ili Simba ineemeke na faida ya mabao ya kufunga.
Simba sasa inakuwa imefikisha pointi 64 ikitanguliwa na Yanga inayoshika usukani wa ligi kwa tofauti ya pointi nne lakini Yanga imecheza mechi 26 hadi sasa wakati Simba imecheza mechi 27.
Kwa hali ilivyo sasa Yanga inahitaji ushindi wa mechi mbili tu ili ifikishe pointi 74 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi hiyo ambayo imebakisha kati ya mechi tatu hadi nne kabla ya kufikia tamati.
Yanga inasubiri kuumana na Singida Alhamisi hii katika mechi nyingine ngumu ambayo Simba itaombea Yanga ipate matokeo mabaya ili walau matumaini ya timu hiyo yaanze kurejea katika mechi zilizobakia.
Soka Namungo yavuruga hesabu za Simba
Namungo yavuruga hesabu za Simba
Read also