Manchester, England
Majanga ya wachezaji majeruhi yanaiandama Man United baada ya kuumia kwa Lisandro Martinez na Raphael Varane katika mechi ya Europa Ligi dhidi ya Sevilla jana Alhamisi, mechi iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Varane alitoka nje wakati wa mapumziko akiwa katika hali iliyotosha kuibua mashaka juu ya majaliwa ya mchezaji huyo wakati Martinez alilazimika kubebwa wakati akitoka nje ya uwanja dakika za majeruhi.
Sevilla ilifunga mabao mawili ya kusawazisha katika dakika 10 za mwisho na kwa sasa kocha wa Man United, Erik ten Hag ana mtihani mgumu wa kupanga kikosi chake kutokana na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza kuwa majeruhi.
Keshokutwa Jumapili Man United itakuwa na mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Nottingham Forest ambapo huenda ikajikuta ikiwakosa Marcus Rashford, Donny van de Beek, Scott McTominay, Luke Shaw na Alejandro Garnacho ambao hali zao ni tete.
Martinez, nyota aliyekuwa na timu ya Taifa ya Argentina iliyobeba Kombe la Dunia Desemba mwaka jana nchini Qatar, alionekana kuwa katika hali mbaya wakati akitoka uwanjani.
Ten Hag hata hivyo hakutaka kuzungumzia undani wa tatizo linalomkabili mchezaji huyo zaidi ya kusema kwamba hatoweza kucheza mechi ya Jumapili.
Kocha huyo hata hivyo alijifariji kuwa na wachezaji wa kuziba nafasi za Martinez na Varane na kuwataja Harry Maguire, Victor Lindelof na Luke Shaw ambaye naye inadaiwa hayuko vizuri.
Man United katika mechi na Sevilla ilipata mabao yake katika dakika 20 za kwanza yaliyofungwa na Marcel Sabitzer na kuonekana kuutawala vizuri mchezo kabla ya kuvurunda katika kipindi cha pili na kuruhusu mabao kupitia Tyrell Malacia na Magire aliyejifunga.
Matokeo mechi za Europa Ligi jana Alhamisi…
Feyenoord 1-0 Roma
B Leverkusen 1-1 Union Saint-Gilloise
Juventus 1-0 Sporting
Man Utd 2-2 Sevilla
Kimataifa Majeruhi waitesa Man United
Majeruhi waitesa Man United
Read also