Na mwandishi wetu
Beki wa kati wa Yanga, Gift Fred (pichani) amesema kuwa anasikia faraja kuvaa jezi ya timu hiyo msimu ujao na hiyo inamfanya kupambana kwa nguvu na akili yake yote kuhakikisha anaitendea haki jezi hiyo.
Nahodha huyo wa zamani wa SC Villa ya Uganda ameeleza kwamba anafahamu juu ya ubora wa wachezaji wenzake hasa mabeki aliowakuta hapo na kuahidi kushirikiana nao ili kuendelea kuwa tishio.
“Nafahamu ukubwa wa Yanga ndio maana nasikia faraja kuvaa jezi ya Yanga msimu ujao na kuipigania uwanjani maana ni timu yenye historia kubwa na juhudi za kutosha, kama ilivyofanya kwenye soka la Tanzania au kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa kufika fainali (Kombe la Shirikisho Afrika),” alisema Gift.
Mchezaji huyo raia wa Uganda amebainisha kuwa haitakuwa kazi nyepesi kwake kudumu ndani ya kikosi cha kwanza cha Wanajangwani hao lakini anaamini atayaweza mapambano hayo ambayo anaamini mwisho yatazaa matunda mema kwa timu nzima kiujumla.
Fred ametua kwenye usajili wa dirisha kubwa kuelekea msimu ujao akiwa ni mahsusi kuja kuimarisha ulinzi kwenye nafasi ya beki wa kati ambayo ina mabeki wengine mahiri; nahodha Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca.