Na mwandishi wetu
Yanga imepanga kwenda na mashabiki Lubumbashi, DR Congo ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi na TP Mazembe na kumaliza wakiwa vinara wa Kundi D katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga inacheza mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi wakiwa vinara wa kundi hilo na pointi zao 10 sawa na US Monastir ya Tunisia lakini miamba hiyo ya Tanzania ipo kileleni kwa idadi kubwa ya mabao ya kufunga.
Kwa jinsi msimamo wa kundi hilo ulivyo, mechi za mwisho ndizo zitakazoamua timu gani itamaliza kinara wa kundi hilo.
Mechi ya Yanga na TP Mazembe inatarajia kupigwa Aprili 2, Lubumbashi nyumbani kwa Mazembe wakati huo Monastir itakuwa nyumbani kwao Tunisia ikivaana na Real Bamako ya Mali.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ameeleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa ushindi katika mchezo huo wamepanga kuwasafirisha mashabiki wao kwenda Lubumbashi kwa ajili ya kutoa sapoti ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
“Tumeanza kuandaa utaratibu maalumu wa kuandaa usafiri kwa ajili ya mashabiki wetu ili kwenda nao Lubumbashi kwa ajili ya mchezo huo sababu mashabiki wetu wamekuwa nguzo muhimu kwa sapoti na dua zao hivyo tumeanza kuratibu jambo hilo, lengo letu ni kuona mchezo wa mwisho unakuwa wa furaha,” alisema Kamwe.
Ofisa huyo ameeleza kuwa kikosi chao kinatarajia kuingia kambini siku mbili zijazo kwa wachezaji ambao hawajaitwa kwenye timu za mataifa yao ili kuanza maandalizi ya mchezo huo.
Kamwe pia kwa niaba ya Rias wa Yanga, Hersi Said amelipongeza benchi lao la ufundi na wachezaji wao kwa jitihada walizozionesha na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Alisema pamoja na mafanikio hayo lakini hawawezi kubweteka sababu kuna kazi kubwa ya kufanya kwenye robo fainali na ikiwezekana kufika fainali ya michuano hiyo.