Munich, Ujerumani
Kocha wa Bayern Munich anayejiandaa kuachana na timu hiyo, Thomas Tuchel amejawa furaha akijivunia kuiwezesha timu hiyo kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuichapa Arsenal bao 1-0.
Ushindi huo unakuwa faraja kubwa kwa kocha huyo anayepitia katika kipindi kigumu cha lawama na shutuma akiwa tayari ametangaziwa rasmi siku ya kuondoka katika timu hiyo baada ya mabosi Bayern kutoridhishwa na utendaji wake.
Arsenal na Bayern ziliumana jana Jumatano usiku katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya ligi hiyo na Bayern kutoka na ushindi wa bao hilo pekee lililofungwa na Joshua Kimmich baada ya sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kwanza.
Katika siku za karibuni Tuchel amekuwa akishutumiwa kwa matokeo mabaya ya timu hiyo ikiwamo kupoteza taji la Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga kwa mara ya kwanza baada ya kuweka rekodi ya kulibeba kwa miaka 11 mfululizo.
Mwenendo mbaya wa timu hiyo uliwafanya mabosi wa Bayern kutangaza hivi karibuni uamuzi wa kuachana na kocha huyo mara baada ya msimu huu.
“Hivyo ndivyo ilivyo, nilijitoa kwa yote tangu siku ya kwanza na nimejitoa hadi siku ya mwisho,” alisema Tuchel ambaye sasa anakuwa kocha wa kwanza Mjerumani mwenye rekodi ya kuzifikisha timu za mataifa matatu tofauti nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, alifanya hivyo na Chelsea mwaka 2021 pamoja na PSG mwaka 2020.
“Nusu fainali ni hatua kubwa, timu nne za mwisho, inafurahisha, ni jambo kubwa furaha na faraja, hii ni hatua ya kipekee, tumeifunga moja ya timu kubwa katika Ligi Kuu England, tunasubiri kuona ushindi huu utakuwa na maana gani kwa klabu hii, msimu hata hivyo bado haujafikia mwisho,” alisema Tuchel.
Tuchel aliongeza kuwa wanajivunia kufikia hatua hiyo kubwa na sasa wanasubiri kuona hali itakavyokuwa katika wiki mbili zijazo kwenye mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Real Madrid.
Wakati huo huo, rais wa Bayern, Herbert Hainer baada ya ushindi dhidi ya Arsenal, alimpongeza Tuchel na kusifia kazi yake akisema kwamba mbinu za kocha huyo zilikuwa za kipekee.
Man City nje
Katika mechi nyingine ya nusu fainali mabingwa watetezi Man City ambao msimu uliopita walibeba mataji matatu, ‘treble’ ndoto zao za kubeba taji hilo msimu huu ziliota mbawa baada ya sare ya bao 1-1 na Real Madrid na hatimaye Real Madrid kusonga mbele kupitia penalti.
Katika mechi hiyo ambayo Man City walikuwa nyumbani Itihad, Real Madrid ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Rodrygo katika dakika ya 12 wakati Man City walisawazisha kupitia kwa De Bruyne dakika ya 76.
Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyopigwa kwenye dimba la Barnebeu, mechi iliisha kwa sare ya mabao 3-3 na hivyo matokea ya jumla kuwa sare ya 4-4 na hatimaye Real Madrid kusonga mbele kwa mikwaju ya penalti 4-3 ambapo waliofunga kwa Real Madrd ni Bellingham, Lucas Vazquez, Nacho Fernandez na Antonio Rudiger wakati Luka Modric alikosa. Kwa City waliofunga ni Julian Alvarez, Phil Foden na Ederson Moraes wakati Mateo Kovacic na Bernado Silva walikosa.
Mechi za nusu fainali zitakazopigwa Aprili 30 na Mei mosi ni kama ifuatavyo
Real Madrid v Bayern Munich
PSG v B.Dortmund