Na mwandishi wetu
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa Sh milioni 200 kwa timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars kwa kufuzu fainali ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcoon 2024) zitakazofanyika Morocco.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro alipokwenda kuwalaki wachezaji na msafara wa timu hiyo Uwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam leo Alhamisi alfajiri walipowasili kutokea Togo kwenye mchezo wa marudiano kufuzu Wafcon.
“Vijana hawa wanastahili pongezi, tumekuja kuwapokea na kuwapongeza na kuleta salamu za Rais Samia Suluhu Hassan, ametangaza bonasi ya Sh milioni 200 kwa vijana hawa, ni habari nzuri kwao na sisi Watanzania,” alisema Dk Ndumbaro.
Naye mkuu wa msafara, makamu wa kwanza wa rais wa TFF, Athuman Nyamlani alishukuru kwa mapokezi na dua za Wanzania na bonasi ya Rais Samia pamoja na msaada wa tiketi walizopewa na serikali.
Twiga Stars imeungana na mataifa mengine 12 baada ya ushindi wa jumla wa mabao 3-2 dhidi ya Togo juzi na kuandika historia ya kufuzu kwa mara ya pili baada ya kufuzu mara ya kwanza mwaka 2010 katika michuano iliyofanyika Afrika Kusini.
Mataifa mengine yaliyofuzu ni wenyeji Morocco, bingwa mtetezi Afrika Kusini, Botswana, Algeria, Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Tunisia, Senegal, Zambia, Mali na Nigeria.