Na mwandishi wetu
Presha ya mchezo wa watani, Simba na Yanga imezidi kupanda kuanzia kwa mashabiki kutokana na hali halisi ya timu hizo kuelekea mchezo huo hasa kwa kukosekana baadhi ya wachezaji muhimu.
Hali hiyo ya presha hasa kwa mashabiki wa timu hizo inatokana na mazingira ya kuelekea mchezo huo yalivyo, timu zote hizo zinakabiliwa na matatizo ya hapa na pale ndani ya vikosi vyao lakini hali hiyo haijazifanya kuacha kujinasibu kupata ushindi.
Yanga inayoonekana kuwa vizuri msimu huu, inatarajiwa kuivaa Simba kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Azam.
Mechi hiyo imekuwa gumzo kutokana na ukubwa wa timu hizo na matokeo waliyokuwa nayo kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Bara msimu huu ambazo ziliisha kwa matokeo ya sare, hivyo mechi ya kesho inategemewa kutoa mbabe.

Kwenye mchezo huo, Yanga itawakosa wachezaji wake walio kwenye ‘form’ kwa sasa; Saido Ntibazonkiza na Dickson Ambundo ambao waliondolewa kambini siku tatu kabla ya mechi hiyo kwa kile kilichoelezwa ni makosa ya utovu wa nidhamu.
Uamuzi wa kuwaondoa wachezaji hao licha ya kudaiwa kufanywa ili kulinda nidhamu katika timu lakini umewanyima raha baadhi ya mashabiki na wana hofu kukosekana kwao kunaweza kuwa chanzo cha tatizo katika mechi hiyo.
Pamoja na hali hiyo, Nabi amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo akieleza kukosekana kwa wachezaji hao hakuwezi kukiathiri kikosi chake kupata ushindi kesho licha ya wachezaji hao kuwa kwenye kiwango kikubwa hivi karibuni.
Kocha huyo pia ameeleza kuwa maandalizi yao yamekwenda vizuri kwa ajili ya mchezo huo huku akiwa tayari kuhakikisha anaibuka na ushindi akiwa hataki kurejea makosa ya mechi mbili ya sare za awali.
“Nafahamu ugumu wa mechi lakini tumejiandaa vizuri, mechi mbili za awali ziliisha kwa kuonekana tulishindwa kuwafunga kwa ajili ya kumtegemea Mayele (Fiston) peke yake lakini sasa najua nini nitakwenda kufanya si vizuri kuzungumza kila kitu lakini tumejipanga,” alisema Nabi.
Simba wao wanatarajia kuikosa huduma ya Shomari Kapombe na kipa Aishi Manula ambao wanadaiwa kuwa ni majeruhi licha ya kuonekana wakifanya mazoezi hivi karibuni.
Kapombe na Manula uwezo wao unajulikana si kwa Simba tu bali hata timu ya Taifa ni wachezaji tegemeo ambao kukosekana kwao kunawatia presha mashabiki wa Simba. Ukimzungumzia Kapombe unamzungumzia beki mwenye uwezo wa kupanda na kupeleka mashambulizi kwa timu pinzani na kwa Manula unamzungumzia kipa bora unamzungumzia Tanzania One, kukosekana kwake ni pigo.
Timu hiyo pia itaikosa huduma ya kiungo wake Clatous Chama ambaye inadaiwa amekwenda kwao Zambia kuhudhuria kumbukumbu ya mwaka mmoja ya kifo cha mkewe.
Pamoja na hali hiyo, Kocha wa Simba, Pablo Franco naye amejinasibu kujiandaa vyema akifahamu ni mchezo mgumu kutokana na ubora wa Yanga kwa sasa wakionekana wako vizuri zaidi yao lakini anaamini kwenye soka lolote linawezekana.
“Mechi ya kesho (Jumamosi) ni mechi nyingine muhimu, ni derby nyingine kwenye michuano ambayo bado tunapambana tukitegemea kuchukua ubingwa. Tunajua ni mchezo mgumu, siwezi kukataa kwamba wao (Yanga) wanaonekana wako vizuri zaidi yetu.
“Wanaonekana wana wakati mzuri na kiwango cha juu uwanjani lakini huu ni mpira na kwenye soka lolote linatokea hasa pale mnapocheza mechi moja ndiyo maana tumekuwa tukijiandaa vya kutosha, tuna mipango kama timu na hata mchezaji mmoja mmoja kuhakikisha tunashinda,” alisema Pablo.
Kabla ya mchezo huo, wakongwe hao walishakutana mara mbili kwenye michuano hiyo na mara zote Yanga imepoteza, ilianza kufungwa mabao 4-1 katika hatua ya nusu fainali ya mwaka 2020 na msimu uliopita ilichapwa tena kwenye fainali kwa bao 1-0, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Wakati Yanga ikijipanga kulipa kisasi kwa kadhia hizo zilizopita, Simba yenyewe inahitaji ushindi ili ipenye fainali na kuutetea ubingwa wake huo angalau ijifute machozi msimu huu kwa kupata kombe moja baada ya kuonekana ligi tayari wameshaipoteza.
Kwenye ligi Yanga inaongoza kwa pointi 64 baada ya mechi 26 dhidi ya pointi 51 za Simba inayoshikilia nafasi ya pili baada ya mechi 25.
