Abidjan, Ivory Coast
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeanza vibaya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya kulala kwa mabao 3-0 mbele ya Morocco.
Ikicheza mechi yake ya kwanza leo Jumatano, Stars iliuanza mchezo huo kwa kasi na kupata kona katika dakika ya tatu kutokana na juhudi za nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta.
Morocco hata hivyo walibadili kibao na kuandika bao la kwanza dakika ya 29 lililofungwa na nahodha wa timu hiyo Roman Sais aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Hakim Ziyech na kipa wa Stars, Aishi Manula kuuokoa kabla ya kumkuta mfungaji.
Morocco baada ya kupata bao hilo walizidi kuonesha uhai wakati kocha wa Stars, Adel Amrouche kwa nia ya kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji, katika dakika ya 35 alimtoa Tarryn Allarakhia na nafasi yake kuingia Simon Msuva.
Msuva aliingia uwanjani kwa kasi na kufanya shambulizi moja ambalo halikuwa tishio kwa Moroccco na hadi timu zinakwenda mapumziko, Morocco walikuwa mbele kwa bao lao moja.
Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwa Stars baada beki Novatus Dismas kupewa kadi nyekundu dakika ya 72 kwa kucheza rafu hali iliyoifanya timu hiyo kubaki na wachezaji 10 uwanjani.
Kadi hiyo ni kama iliipunguzia nguvu Stars ambayo ilijikuta ikipachikwa bao la pili katika dakika ya 78 lililofungwa na Azidin Ounai ambaye alilipika bao hilo baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Stars na kutoa pasi ambayo baadaye alirudishiwa na hatimaye kuujaza mpira wavuni.
Dakika mbili baadaye Youssef En-Nesyri aliipatia Morocco bao la tatu akiunganisha pasi ya chinichini ya Achraf Hakimi na kupiga shuti ambalo lilipita miguuni kwa Manula, bao ambalo awali lilizua utata kwa kilichoonekana kuwa mfungaji aliotea lakini baadaye mwamuzi aliamuru mpira uwekwe kati na mfungaji kushangilia akiwa kwenye benchi baada ya kuwa tayari alishafanyiwa mabadiliko na kocha wake.
Wakati Stars ikiwa nyuma kwa bao 1-0, kocha Amrouche alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Samatta na nafasi yake kuingia Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mudathir Yahya na nafasi yake kuingia Morris Abraham.
Mabadiliko hayo hata hivyo hayakuwa na madhara yoyote kwa Morocco zaidi ya kuimarisha uhai wa Stars kwa kuongeza idadi ya pasi ambazo hata hivyo zilikaribia kwa nadra lango la Morocco.
Katika mechi hiyo, wachezaji wawili wa Stars, Himid Mao na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr walipewa kadi za njano kwa kucheza rafu.
Stars iliyo kundi F sasa imebakiwa na mechi mbili dhidi ya Zambia na DR Congo, mechi ambazo zitaamua hatma ya timu hiyo kama itasonga mbele au kuishia hatua ya makundi.
Kimataifa Morocco yaipiga Stars 3-0 Afcon
Morocco yaipiga Stars 3-0 Afcon
Read also
