Na mwandishi wetu
Baada ya kiungo wa Taifa Stars, Novatus Dismas kusajiliwa na klabu ya SV Zulte Waregem ya Ligi Kuu Ubelgiji, Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohamed Mchengerwa amepongeza usajili huo na kumtaka mchezaji huyo kuweka uzalendo mbele.
Nova amekamilisha dili hilo la kandarasi ya miaka mitatu akitokea kwa vigogo wa Israel, Macabi Tel Aviv na sasa anaungana na Mtanzania, Kelvin John anayekipiga KRC Genk ya nchini humo pia.
Mchengerwa mbali na kumpongeza lakini pia alimsisitiza kuendelea kuuweka uzalendo wa taifa mbele na nidhamu ili kuzifikia ndoto za soka alizonazo na kuliheshimisha taifa pia kupitia yeye.
“Hongera sana kijana Novatus Dismas kwa kukamilisha usajili kwenda klabu ya Zulte Waregem. Kusogea kwake kwenye Ligi ya Ubelgiji ni hatua kubwa sana katika maisha yake na muhimu kwa Serikali yetu.
“Hii ikiwa ni sehemu ya mpango wa wizara kuhakikisha vijana wengi wanapata fursa katika ligi za Ulaya zilizosogea katika soka ili muweze kuwa msaada kwa Taifa kuwakilisha nchi. Endelea kukumbuka maneno yangu, uzalendo kwa taifa lako uweke mbele, uwe na nidhamu na Mwenyezi Mungu akubariki katika kila hatua unayopiga,” alieleza Mchengerwa.
Nova alianza kuonekana kwa mara ya kwanza na kikosi cha Azam chini ya miaka 19 na kuibuka mchezaji bora chipukizi wa ligi msimu wa 2019-20 akiwa Biashara United kwa mkopo kabla ya kurejea Azam na kuuzwa Macabi msimu wa 2020-21 kabla ya juzi kutua Waregem.
Waregem mabingwa mara mbili wa Kombe la FA Ubelgiji, walimtambulisha mchezaji huyo rasmi jana usiku kwa namna ya kipekee kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii katika kuendelea kukisuka kikosi chao kuelekea msimu wa 2022-23.
Soka Waziri apongeza usajili wa Dismas Ubelgiji
Waziri apongeza usajili wa Dismas Ubelgiji
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
