Manchester, England
Kipa wa Man Utd, Andre Onana atalazimika kuondoka katika kambi ya timu ya taifa ya Cameroon ili kwenda Manchester kuangalia ukubwa wa majeraha aliyoyapata wakati akiiwakilisha Cameroon kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.
Onana alitolewa dakika ya 81 wakati Cameroon ikiumana na Mauritius na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 lakini kipa huyo hakuwa na muda kufurahia ushindi huo baada ya kuumia akiwa katika harakati za kuokoa goli.
Maofisa wa timu ya taifa ya Cameroon hata hivyo hawakuwa tayari kuelezea ukubwa wa maumivu aliyoyapata Onana katika mechi hiyo iliyopigwa Ijumaa iliyopita.
Onana alisajiliwa na Man United Julai mwaka huu akitokea Inter Milan ya Italia kwa ada ya Pauni 47.2 milioni na tayari ameiwakilisha timu hiyo katika mechi 18 za mashindano tofauti akiwa ndiye kipa namba moja tangu kuondoka kwa David de Gea.
Man United yenye rundo la wachezaji majeruhi baada ya mapumziko ya kalenda ya Fifa itaingia uwanjani Novemba 26 kuumana na Everton na siku tatu baadaye itaikabili Galatasaray katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wachezaji wa Man United ambao ni majeruhi kwa sasa ni Casemiro, Christian Eriksen, Jonny Evans, Tyrell Malacia, Rasmus Hojlund, Lisandro Martinez, Luke Shaw na Aaron Wan-Bissaka.
Kimataifa Onana aongeza idadi ya majeruhi Man Utd
Onana aongeza idadi ya majeruhi Man Utd
Read also