Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Hans Pluijm ameamua kuua ndege wawili kwa jiwe moja baada ya kuanza mapema kuichunguza Future FC ya Misri, timu anayotarajia kukutana nayo kama tapenya kwenye hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pluijm ameeleza hayo ikiwa ni siku moja imepita tangu aliposema ameanza kuifuatilia timu ya JKU ya Zanzibar atakayokutana nayo kwenye hatua ya awali ya michuano hiyo.
Kocha huyo raia wa Uholanzi amebainisha kuwa mshambuliaji wao, Kazadi Kasengu aliyewahi kukipiga Misri katika timu za El Masry na Gaish kabla ya kutua Singida msimu uliopita amekuwa akiwaeleza mbinu, udhaifu, ujanja na mazingira mengine juu ya wapinzani wao hao watarajiwa.
“Sina mengi kwa sasa ninayoyafahamu kuhusu Future lakini Kazadi amekuwa akinieleza machache na mengine mengi nitaendelea kuyafahamu kuhusu wao, najua tu kwamba wana timu nzuri, wako sawa lakini yapo mengine nitahitaji kuyajua.
“Mechi ya JKU ni muhimu sana kwa sasa kwetu maana hatuwezi kufika kwa Future mpaka tuvuke hapa lakini si vibaya kufahamu kuhusu Future pia, naamini taratibu nitaendelea kuwafahamu kwa kupitia Kazadi pia,” alisema Pluijm.
Singida inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo baada ya kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa wametoka kupanda daraja msimu wa 2021-22.