Na mwandishi wetu
Bao pekee la dakika za lala salama limeizamisha Simba katika mechi yake ya tatu ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Waydad AC ya Morocco, mechi iliyopigwa Jumamosi hii usiku.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kuburuza mkia katika kundi lake ikiwa na pointi mbili katika kundi ambalo linaongozwa na Asec Memosa ya Ivory Coast ikifuatiwa na Jwaneng Galaxy na Waydad ni ya tatu.
Waydad, waliokuwa wenyeji wa mchezo huo bao lao pekee lilifungwa na Zakaria katika dakika tatu za nyongeza na lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa juu na kuwapita mabeki wa Simba kabla ya kumkuta mfungaji.
Zakaria alifumua shuti kali la mguu wa kushoto na mpira kupita miguuni mwa kipa wa Simba, Ayoub Lakred na kuibua shangwe kwa mashabiki na wachezaji wa Waydad waliofurahia ushindi wa kwanza wa timu yao kwenye hatua ya makundi.
Lakred licha ya kufungwa bao hilo, alionesha umahiri wa kuokoa michomo kadhaa iliyoelekezwa langoni mwake ukiwamo mkwaju wa penalti iliyotolewa dakika ya 38 baada ya Kibu Denis kumchezea rafu Seifdin.
Mpigani wa penalti hiyo, Yahya Jabrane anayesifika kwa umahiri katika mikwaju ya penalti, alishindwa kumchambua Lakred ambaye aliokoa shuti la chichini lililopigwa upande wake wa kulia na mpira kurudi ndani lakini Waydad walishindwa kuutumia kupata bao.
Simba ilianza kuonesha makali yake dakika ya 23 baada ya Saido Ntibazonkiza kupiga mpira wa adhabu ambao uliokolewa na kumkuta Sadio Kanoute ambaye naye mpira wake uliokolewa na kumkuta Onana ambaye naye hakuweza kuipa Simba bao.
Waydad walijibu mapigo dakika mbili zilizofuata baada ya Bouly Sambu kuwatoka kwa kasi mabeki wa Simba na kufumua shuti ambalo hata hivyo halikuzaa matunda.
Dakika ya 43 Onana aliuwahi mpira wa juu langoni mwa Waydad na kuupiga kichwa kabla ya kumkuta Mohamed Hussein Zimbwe Jr ambaye naye alipiga shuti lililookolewa kabla ya Kanoute kujichanganya wakati akipiga mpira na Simba kupoteza nafasi hiyo.
Kocha wa Simba Abdulhak Benchikha alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Willy Onana na nafasi yake kuingia Clatous Chama na baadaye akawatoa Kibu na Kanoute na nafasi zao kuchukuliwa na Muzamiru Yassin na Moses Phiri.
Zikiwa zimebakia dakika chache mpira kumalizika, Benchikha pia aimtoa Saido na nafasi yake kuchukuliwa na Luis Miquissone, mabadiliko ambayo licha ya kuongeza uhai kwa Simba lakini hayakuweza kuipatia timu hiyo bao.
Matokeo hayo yanawafanya wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu mahasimu za Simba na Yanga zote kuburuza mkia kila moja ikiwa na pointi mbili katika mechi tatu.
Kimataifa Waydad yaizamisha Simba
Waydad yaizamisha Simba
Read also