Na mwandishi wetu, Kagera
Kagera Sugar leo Jumatano imeibana Simba kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba baada ya kuilazimisha sare ya bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu NBC.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kuendelea kushika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo ikiwa na pointi 38 baada ya mechi 17 sawa na Azam ambayo inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37 wakati Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 44.
Kagera ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 15 lililofungwa na Deus Bukenya lakini Simba ilisawazisha bao hilo dakika saba kabla ya mapumziko mfungaji akiwa ni Henock Inonga na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare, matokeo ambayo yaliendelea kuwa hivyo hadi dakika 90 za mchezo zinatimia.
Matokeo hayo hata hivyo yanaweza yasiwe mazuri kwa baadhi ya mashabiki wa Kagera wakikumbuka Januari 26 mwaka huu timu hizo zilipokutana kwenye uwanja huo huo katika ligi msimu uliopita ambapo Kagera ilitoka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Hamis Kiiza.
Kagera sasa imefikisha pointi 23 ikiwa inashika nafasi ya sita ikifuatiwa na Geita Gold inayoshika nafasi ya saba ikiwa pia na pointi 23 lakini imezidiwa na Kagera kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, timu zote hizo zimecheza mechi 17 hadi sasa.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo, Prisons ilitoka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Dodoma Jiji wakati Azam ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na Geita Gold.
Soka Simba yabanwa Kagera
Simba yabanwa Kagera
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
