Na mwandishi wetu
Licha ya Mashujaa FC kuwa na hali mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC, lakini wamewaahidi mashabiki wao kuwa hawatashuka daraja na katika kudhihirisha hilo wataanza na ushindi kwenye mechi yao ijayo dhidi ya Yanga SC.
Hayo yameelezwa Jumatatu hii na kocha msaidizi wa Mashujaa, Makata Maulidi baada ya matokeo ya suluhu dhidi ya Singida FG kwenye mchezo uliopigwa jana Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kufanya wasogee mpaka nafasi ya 13 kwa pointi 23 baada ya mechi 24.
“Mechi ilikuwa ngumu sababu mechi yoyote ya ugenini, mwenyeji anaamini atapata pointi tatu lakini Singida walitufunga mchezo wa kwanza (3-1) kwa hiyo tukaweka mpango wa namna ya kucheza nao na kujaribu kupambana lakini haikuwa riziki yetu, tumepata sare.
“Lakini hayo yamepita na sasa tunatazamia zaidi mechi ya Yanga inayofuata kule Kigoma, tunajua hatupo katika nafasi nzuri, tunataka kuona namna ya kutoka tulipo kwa hiyo yeyote ambaye yupo mbele yetu, tukicheza naye lazima tupate matokeo kwake.
“Tuwaambie na kuwahamasisha mashabiki wasikate tamaa, timu yetu haiwezi kushuka daraja, tutapambana kubaki ligi kuu kuhakikisha tunawapa burudani zaidi msimu ujao,” alisema Maulid.
Mashujaa iliyopanda kushiriki Ligi Kuu NBC msimu huu, imebakiza mechi sita kufunga pazia la ligi ambapo ikishaumana na Yanga Mei 8, itavaana na KMC, Tabora United, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar kisha itamalizana na Dodoma Jiji.