Na mwandishi wetu
Licha ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kufurahishwa na mechi za hisani kwa jamii lakini amewataka wadau na wadhamini mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizo.
Karia amezungumza hayo baada ya juzi kushuhudia mchezo wa hisani wa Wape Tabasamu uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro ambapo Team Job iliyokuwa ikiundwa na Dickson Job iliibuka na ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Team Kibwana ya Kibwana Shomari.
“Malengo ambayo yanatakiwa ule mchezo yalifikia maana uwanja ulijaa na wengine wakachangia ambao hawakuja uwanjani, lakini malengo yamefikiwa na niwapongeze wachezaji hawa wamekusanyika kuja kusapoti jambo ambalo ni la jamii.
“Ni kitu kikubwa hicho maana wametumia muda wao wa mapumziko kusapoti jamii kuliko ambavyo kila mmoja angeenda kivyake lakini wameamua kuja kuchangia jamii na walioanzisha hili wazo ni jema na tuwaombee na liende kufanya makubwa walikodhamiria kupeleka,” alisema Karia na kuongeza:
“Kwa hiyo wanachofanya ni jambo jema zaidi, na taasisi mbalimbali ziwadhamini kwenye mikoa mingine waweze kwenda na kurejesha kwa jamii kwa pamoja, kwa hiyo wakati mwingine watu wawadhamini ili wafanye bora zaidi hili jambo kwa jamii.”
Karia pia aliwapongeza wachezaji wengine walioshirikiana kwenye kipindi hiki cha mapumziko kucheza mechi hizo kama vile walivyofanya Feisal Salum na Abdulaziz Makame kule Zanzibar au Bakari Mwamnyeto na Zawadi Mauya walipokuwa Mbeya.
Soka Karia apongeza mechi za hisani
Karia apongeza mechi za hisani
Read also
