Na mwandishi wetu
Michuano ya soka ya ligi ya klabu chini ya miaka 20 (U20) inafikia tamati kesho Jumapili kwa mchezo wa fainali kati ya Mtibwa Sugar na Geita Gold kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kuelekea mchezo huo utakaoanza kuunguruma saa 12.00 jioni, Kocha Mkuu wa Mtibwa, Awadh Juma alisema anafahamu ugumu wa fainali, akiamini itakuwa mechi nzuri ingawa watachanga karata zao vizuri kuhakikisha wanautetea ubingwa huo.
“Naamini itakuwa mechi nzuri, ngumu sababu Geita tangu waanze mashindano wamekuwa kwenye mtiririko mzuri lakini tunahitaji kuwa bora zaidi ili kuhakikisha tunalinda ubingwa wetu maana tunaokwenda kucheza nao wako vizuri,” alisema Juma.
Alisema hawezi kusema wanakwenda kujiongeza vipi kwani wanafahamu hata Geita nao wanajipanga vilivyo kuivaa timu yao ambayo kila wakati imekuwa ikionesha umakini kwenye michuano hiyo.
Kocha wa Geita, Choke Abeid alisema: “Ni mara ya kwanza tunaingia fainali, lakini fainali ni fainali na mashindano haya ni magumu kiujumla lakini naamini fainali itakuwa ngumu sana na hatumhofii yeyote sababu lazima tuendelee kupambania mipango tuliyonayo.”
Mtibwa ilitinga fainali kwa kuibugiza Azam FC mabao 2-1 wakati Geita iliingia fainali kwa kuichapa Kagera Sugar mabao 2-0.
Kabla ya mchezo wa fainali, saa 9.00 alasiri, Azam itavaana na Kagera Sugar katika uwanja huo huo kuwania nafasi ya tatu.
Soka Mtibwa, Geita kukiwasha fainali U20
Mtibwa, Geita kukiwasha fainali U20
Related posts
Read also