Na mwandishi wetu
Yanga kama walivyo mahasimu wake Simba wote wameishia hatua ya makundi ligi ya mabingwa Afrika msimu wa 2025-26 huku Yanga ikiishia hatua hiyo kibabe kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie ya Algeria.
Matokeo ya mchezo huo wa Kundi B uliopigwa leo Jumapili Februari 15, 2026 Uwanja wa Amaan, Zanzibar, bado hayakuweza kuibeba Yanga kwani licha ya kufikisha pointi nane, imezidiwa pointi moja na AS FAR Rabat ya Morocco.
Rabat ambayo nayo leo ilikuwa uwanjani dhidi ya Al Ahly ya Misri imetoka sare ya bila kufungana, matokeo ambayo yametosha kuifanya Rabat iungane na Al Ahly yenye pointi 10 ambayo pia ndio kinara wa kundi hilo.
Ushindi wa Yanga ulianza kupatikana dakika ya 38 kwa bao la Depú alilofunga kwa mkwaju wa penalti ambayo ilitolewa na mwamuzi baada ya Pacome Zouzoua kuchezewa rafu.
Kipindi cha pili Yanga waliongeza kasi ya mashambulizi na kuandika bao la pili dakika ya 62 mfungaji akiwa Depu tena safari hii akiruka juu na kuuwahi mpira wa kona kabla ya kuujaza wavuni kwa kichwa.
Dakika zisizozidi tatu baada ya bao hilo, Yanga waliongeza bao la tatu na la mwisho lililofungwa na beki wa kushoto wa timu hiyo, Shadrack Boka akiitumia vizuri pasi ya Prince Dube.
Wawakilishi wengine wa Tanzania Azam FC nao wameaga rasmi michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushindwa kutamba ugenini wakichapwa mabao 2-0 na Waydad ya Morocco.
Baada ya Azam na Yanga kukwama, Tanzania sasa inabaki bila mwakilishi katika michuano ya klabu barani Afrika kwa msimu huu wa 2025-26 na sasa timu hizo zinapaswa kuanza hesabu za msimu ujao wa 2026-27.
Kimataifa Yanga yaaga kibabe ligi ya mabingwa
Yanga yaaga kibabe ligi ya mabingwa
Read also
