Na mwandishi wetu
Kipa namba mbili wa Yanga, Metacha Mnata (pichani) amesema atatumia mchezo wa TP Mazembe kumshawishi kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kumpanga kikosi cha kwanza.
Kipa namba moja wa timu hiyo, Djigui Diarra ataukosa mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mazembe utakaopigwa Aprili 2, mwaka huu mjini Lubumbashi.
Kipa huyo ameeleza kuwa tangu arejee kwa mkopo katika kikosi hicho kwenye dirisha dogo msimu huu, amejifunza mengi kutoka kwa Diarra hivyo anaamini yupo tayari kuidakia timu yake katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho na kuonesha kiwango kikubwa.
“Najua kocha nini anataka nifanye lakini natambua timu yangu inahitaji nini katika mchezo huo kwa hiyo nipo tayari, ukizingatia uzoefu wa kucheza mechi hizi za kimataifa ninao na sina presha,” alisema Metacha.
Kipa huyo ameeleza kuwa si kitu rahisi kucheza na Mazembe wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani bila kuruhusu bao lakini kwake atapambana kwa kushirikiana na wachezaji wenzake ili asiruhusu bao.
Alisema endapo hilo litafanikiwa anaamini atafanikiwa kubadilisha mawazo ya kocha wake na ataanza kumtumia kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa kabla hajatimka kwenye timu hiyo misimu miwili iliyopita na kutua Polisi Tanzania.
Metacha ambaye anacheza kwa mkopo wa miezi sita akitokea Singida Big Stars, amesema matumaini yake ni kuendelea kubaki kwenye kikosi cha miamba hiyo ya soka nchini kwa uongozi kumpa mkataba wa kudumu.