Na mwandishi wetu
Simba imeitoa Pamba ya Mwanza katika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Azam kwa kuichapa mabao 4-0 na sasa inasubiri kuumana na mahasimu wao Yanga katika mechi ya nusu fainali.
Simba ilipata ushindi huo jana katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa baada ya kuhaha katika dakika 43 za mwanzo kwa kuishambulia Pamba lakini washambuliaji wa Simba walikosa umakini katika umaliziaji.
Simba ilianza kuandika bao lake la kwanza dakika moja kabla ya timu hizo kwenda mapumziko mfungaji akiwa ni Peter Banda, bao ambalo lilionekana kuikatisha tamaa Pamba ambayo juhudi zao za kujihami zilikwama katika kipindi cha pili walipojikuta wakiendelea kupachikwa mabao zaidi.
Dakika tatu baada ya kuanza kipindi cha pili, Simba waliandika bao la pili, mfungaji akiwa ni Kibu Dennis ambaye aliitumia vizuri krosi ya Shabalala. Hali ilizidi kuwa mbaya kwa Pamba ambayo ilipachikwa mabao mengine mawili katika dakika za 53 na 89, mfungaji akiwa ni Yusuf Mhilu.
Pamba ni kama vile ilidhamiria kucheza mpira wa kujihami zaidi na kutafuta bao la kushtukiza kwani katika dakika 15 za mwanzo kazi yao ilikuwa kuzuia mashambulizi ya Simba ambayo ilipiga mashuti sita huku Pamba wakishindwa kufanya shambulizi lolote tishio langoni mwa Simba.
Na hadi timu zinakwenda mapumziko, Pamba walipiga shuti moja tu la maana langoni mwa Simba huku wachezaji wa Simba, John Boco, Kibu na Banda wakishindwa kuzitumia nafasi ambazo zingeweza kuwapatia mabao ya mapema.
Baada ya ushindi huo, mashabiki sasa wanasubiri kuiona timu hiyo ikiumana na mahasimu wao, Yanga katika mechi ya nusu fainali ambayo itapigwa mapema mwezi ujao, hiyo ni baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika mechi mbili zilizopita.
LigiKuu Simba yaiua Pamba, Dar Derby hiyoo
Simba yaiua Pamba, Dar Derby hiyoo
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
