Na mwandishi wetu
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC, Yanga wameendelea kuimarisha kikosi chao kwenye dirisha hili la usajili baada ya kudaiwa kuinasa saini ya winga wa Ghana, Augustine Okrah kwa mkataba wa miaka miwili.
Mchezaji huyo ambaye makabrasha yake yanaonesha ana umri wa miaka 30, amejiunga na Yanga akiwa kinara kwenye kiwango bora katika chati ya wafungaji wa Ligi Kuu Ghana akiwa amefunga mabao manane.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka nchini Ghana, inadaiwa nyota huyo kutoka klabu ya Bechem United amesaini Jangwani kwa dau la Dola za Kimarekani 150,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 375.
Inaelezwa kuwa Okrah aliyewahi kukipiga Simba alitua nchini tangu jana Alhamisi kukamilisha taratibu za kuichezea timu hiyo inayovaa jezi ya kijani na njano na tangu wakati huo amekuwa akijadiliwa kama kweli amejiunga na Yanga au la.
Huu unakuwa usajili wa pili kwa Yanga kwenye kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili baada ya kuinasa saini ya kiungo Shekhan Ibrahim Khamis kutoka JKU ya Zanzibar kwa mkataba wa miaka mitatu.
Akizungumza leo Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema kifaa kipya ni ‘mgeni’ mwenyeji aliyetakiwa kutambulishwa leo Ijumaa lakini Rais wa klabu hiyo, Hersi Said ameagiza wakamtambulishe visiwani Zanzibar.
“Huyu mchezaji ni mgeni lakini mwenyeji tunatarajia kumtambulisha katika mchezo wetu wa kwanza, utambulisho wake utafunika ile shoo ya msanii Diamond (Platnumz) aliyoifanya pale Uwanja wa Amaan Complex.
“Usajili ambao unafanywa ni kulingana na mapendekezo ya kocha Gamondi (Miguel) kuhakikisha tunaimarisha kikosi chetu na kuwa imara zaidi,” alisema Kamwe.
Aliongeza kuwa timu inaondoka leo kuelekea Zanzibar huku wakiwa na dhamira ya kutwaa Kombe la Mapinduzi na kwenda na kikosi cha wachezaji wote isipokuwa wale walioko katika timu za taifa.
Nyota wengine wanaotajwa kusajiliwa na Yanga ni Simon Msuva na mshambuliaji kutoka klabu ya Dynamo Dougla ya Cameroon, Leonel Ateba.
Soka Hadithi ya Okrah Yanga yapamba moto
Hadithi ya Okrah Yanga yapamba moto
Read also