Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema hana presha kuelekea mchezo wao dhidi ya Simba au Dar Derby kutokana na ubora wa kikosi chake pamoja na maandalizi mazuri wanayoyafanya.
Mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kutokana na upinzani mkali uliopo baina ya timu hizo za Kariakoo jijini Dar es Salaam unatarajia kuchezwa Novemba 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa.
Gamondi alisema anachokifanya ni kupandikiza mbinu zitakazowapa pointi tatu katika mchezo huo na siyo kutumia muda wake kuwazungumzia wapinzani wao kitu ambacho kitawapa presha wachezaji wake.
“Sitaki kuuzungumzia sana sababu ni mchezo wa kawaida kama ilivyo mechi nyingine zilizopita dhidi ya KMC au JKT, kinacholeta upekee hapo ni neno ‘derby’, ambalo kwa kweli nina uzoefu na mechi hizi, tunaendelea na maandalizi ikiwemo kupandikiza mbinu bora kwa wachezaji lengo ni kupata pointi tatu,” alisema Gamondi.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema siku zote mtazamo wake umekuwa ni kujenga timu inayocheza kwa muunganiko na ushirikiano na siyo mchezaji mmoja mmoja na anafurahi kuona hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa ndio maana hana presha kuelekea mchezo huo.
Alisema kama yeye anavyoona, hiyo ni mechi ya kawaida ndivyo amewataka wachezaji wake waone hivyo ili wasije kupania na kujikuta wakishindwa kutimiza kile ambacho amewaelekeza kwenye mchezo huo.
Alisema kwamba kwenye mchezo huo anahitaji ushindi ili kulipiza kisasi baada ha kufungwa na Wekundu hao kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.
Endapo Yanga itashinda mchezo huo dhidi ya Simba, Gamondi atakuwa ameweka rekodi ya kuzifunga timu zote kubwa zinazofukuzia ubingwa baada ya wiki iliyopita kuifunga Azam FC mabao 3-2.