Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba ipo katika hatua za mwisho kumalizana na Radhi Jaidi (pichani) raia wa Tunisia kuwa kocha wao mkuu akichukua nafasi ya Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyefutwa kazi wiki mbili zilizopita.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya Jaidi na mabosi wa Simba yamefikia pazuri na muda wowote kuanzia leo Jumatatu wanaweza kumtambulisha kocha huyo.
Mara baada ya kutambulishwa kocha huyo anatarajia kuanza majukumu ya kukinoa kikosi hicho ambacho Jumamosi hii kinakabiliwa na mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Awali uongozi wa Simba, ulianzisha mazungumzo na aliyekuwa kocha wa RC Belouizdad ya Algeria, Abdelhak Benchikha lakini walishindwana kutokana na kiasi kikubwa cha mshahara ambacho kocha huyo alikuwa akihitaji na ndipo uongozi wa Simba ukaamua kuachana naye na kutua kwa Jaidi.
Kitu kikubwa ambacho mabosi wa Simba wamevutiwa nacho kutoka kwa kocha huyo mwenye leseni ya UEFA Pro ni uzoefu aliokuwa nao katika kufundisha ligi mbalimbali Barani Ulaya, Asia na Marekani.
Mbali na hayo pia Jaidi amepata mafanikio makubwa wakati akiwa mchezaji anayemudu nafasi ya beki wa kati na kushinda mataji kadhaa akiwa na timu ya taifa ya Tunisia pamoja na klabu alizochezea.
Historia inaonesha Jaidi mwenye umri wa miaka 48 kabla ya kugeukia kwenye kazi ya ukocha amewahi kuitumikia Esperance pia mwaka 2004 aliisaidia timu ya taifa ya Tunisia kubeba taji la Afcon.
Baada ya hapo Jaidi alihamia England ambako alichezea klabu za Bolton, Birmingham na Southampton na baada ya kustaafu aligeukia ukocha ambapo baada ya kuhitimu mafunzo, uongozi wa klabu ya Southampton ulimpa kazi ya kuwa kocha mkuu wa timu ya vijana chini ya miaka 23.
Pia Jaidi amewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Hartford Athletic inayoshiriki Ligi ya Marekani (USL Championship) pia amewahi kufundisha timu ya Cercle Brugge ya Ubelgiji akiwa kocha msaidizi.
Baada ya kutoka Ubelgiji alirudi kwao Tunisia na kuinoa timu ya Esperance na msimu uliopita alifanikiwa kuipa ubingwa wa taji la Super Cup kwa kuifunga CS Sfaxien na kisha kuachana nayo.
Soka Kocha Mtunisia asubiriwa Simba
Kocha Mtunisia asubiriwa Simba
Related posts
Read also