Na mwandishi wetu
Kocha Nasreddine Nabi hatimaye ameamua kuachana na klabu ya Yanga huku kukiwa na habari kwamba anaenda kujiunga na klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Uamuzi huo wa Nabi unakuwa umefuta mjadala uliotawala siku za hivi karibuni miongoni mwa wadau wa soka kuhusu majaliwa ya kocha huyo kama angeongeza mkataba au angeamua kuondoka.
Awali Jumtano hii, GreenSports ilimnukuu Makamu Rais wa Yanga, Arafat Haji akisema kwamba walitarajia kukutana na kocha huyo Alhamisi ili kujadili suala la kumuongezea mkataba.
Hata hivyo saa kadhaa baada ya kauli ya kiongozi huyo, uongozi wa Yanga kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo ulitoa taarifa rasmi ya kuagana na kocha huyo.
Taarifa hiyo ilidai kuwa uongozi wa Yanga umefikia makubaliano ya kuachana na Nabi baada ya kocha huyo mwenyewe kuomba kutoongeza mkataba na klabu hiyo.
Mkataba wa Nabi pamoja na sehemu kubwa ya jopo lake kwenye benchi la ufundi umefikia ukomo mwishoni mwa msimu huu na awali yalikuwapo matarajio makubwa kwa kocha huyo kuongeza mkataba.
Uongozi wa Yanga umemshukuru kocha huyo kwa kipindi chote ambacho amekuwa na timu hiyo ba kumtakia heri katika majukumu yake mapya ingawa haijaeleweka kuhusu wajumbe wengine wa benchi la ufundi waliokuwa wakisaidiana na kocha huyo.
Nabi ataendelea kukumbukwa katika klabu ya Yanga kwa kuiwezesha timu hiyo kubeba mataji mawili ya Ligi Kuu NBC, mawili ya Kombe la FA (ASFC) pamoja na mataji mawili ya Ngao ya Jamii.
Kocha huyo pia ataendelea kukumbukwa kwa kuweka rekodi ya kuifikisha kwa mara ya kwanza timu hiyo katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na ingawa hakujawa na taarifa rasmi za kocha huyo kwenda Kaizer Chiefs, duru za kimichezo katika siku za karibuni zimeripoti kuwa klabu hiyo imekuwa ikimuwinda Nabi kutokana na mafanikio ambayo ameyapata akiwa Yanga.
Soka Nabi aondoka Yanga
Nabi aondoka Yanga
Read also