Na mwandishi wetu
Imebainika kuwa kurejea kwa beki wa kulia Simba, David Kameta ‘Duchu’ (pichani) kumepelekea beki mwingine wa kulia wa timu hiyo, Israel Mwenda kupewa majukumu mapya ya kucheza beki wa kushoto.
Ujio wa Duchu Simba, umefanya mabeki wa kulia kuwa watatu pamoja na Shomari Kapombe na hivyo kuibua sintofahamu juu ya matumizi ya watatu hao lakini imefafanuliwa kuwa Israel sasa atasaidiana na beki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa hata benchi la ufundi chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ linafahamu ubora alionao Mwenda kwenye majukumu ya beki wa kushoto hasa alipoonesha kwenye mechi za mwisho msimu uliopita.
“Yupo Kapombe, beki mbili bora kuwahi kutokea Tanzania, yupo Israel Mwenda na pia tumemrejesha kundini Kameta kijana wetu, sababu kubwa ni kuendelea kuimarisha timu yetu maana tunashiriki michuano mingi msimu ujao.
“Lakini Mwenda ana uwezo mkubwa na kama umeangalia hivi karibuni amekuwa na uwezo wa kucheza vile vile upande wa kushoto hivyo anaweza kumsaidia Hussein lakini anaweza kucheza namba ya uhalisia kwa maana ya namba mbili, hivyo ni faida kitimu,” alisema Ally.
Simba ambayo imesafiri leo Jumanne kuelekea Uturuki kuweka kambi ya maandalizi msimu ujao mpaka sasa imetambulisha wachezaji wanne; Willy Onana, Che Malone Fondoh, Aubin Kramo na Duchu.
Timu hiyo pia imewaongezea mikataba mabeki wake, Kapombe na Zimbwe Junior ambao sasa watakuwa na timu hiyo hadi mwaka 2025.
Soka Duchu ambadili Mwenda Simba
Duchu ambadili Mwenda Simba
Read also