Na mwandishi wetu
Kikosi cha wachezaji 23 wa Singida Fountain Gate kimekwea pipa jioni ya leo Jumanne kuelekea Cairo, Misri tayari kwa mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future FC ya Misri utakaopigwa Oktoba Mosi, mwaka huu.
Timu hiyo itavaana na Future katika mechi ya mkondo wa pili wa raundi ya kwanza kuwania kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo, mechi itakayoanza majira ya saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Al-Salam, Cairo.
Singida itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya awali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza (pichani juu) ameeleza kuwa benchi la ufundi chini ya kocha Mathias Lule linaamini juu ya maandalizi ya kikosi hicho kuelekea mchezo huo wakiwa tayari kutafuta matokeo ugenini.
“Tunataka kumaliza tulichokianza Dar es salaam kwa hiyo kiujumla maandalizi yalikuwa makubwa na kocha ana imani kubwa na kikosi kwa ajili ya kuhakikisha tunatafuta matokeo na tunasonga hatua inayofuata,” alisema Masanza.