Na mwandishi wetu
Vigogo wa soka la Tanzania, timu za Simba na Yanga wametoka sare ya bila kufungana katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa usiku wa Jumapili, Machi Mosi, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Kwa matokeo hayo, Yanga wameendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakifikisha pointi 29 na Simba kushika nafasi ya tatu na pointi zao 24, timu zote hizo kila moja imeshacheza mechi 11.
Matokeo hayo pia yanaifanya Yanga kufikisha mechi ya saba mfululizo bila kufungwa na Simba ingawa matokeo ya sare siyo yaliyotegemewa na mashabiki walio wengi wa timu hiyo bingwa mtetezi wa ligi.
Simba waliuanza mchezo kwa kasi na katika dakika 10 za mwanzo walionesha dhamira yote ya kufuta uteja wa mechi saba zilizopita kwa kutengeneza nafasi kadhaa langoni mwa Yanga lakini hazikuzaa matunda.
Shambulizi la kwanza kabisa la kutisha la Simba langoni mwa Yanga lilifanyika dakika ya nne baada ya Jospin Loemba kuinasa pasi ya Nickson Kibabage na kufumua shuti lakini kipa Djigui Diarra alikuwa makini na kuokoa mpira huo.
Nao Yanga walijibu shambulizi hilo dakika tano baadaye, Mohamed Damaro akiwa katika nafasi nzuri aliufumania mpira na kufumua shuti ambalo hata hivyo lilitoka nje ya lango la Simba.
Katika dakika ya 70, Simba walifanya shambulizi la maana langoni mwa Yanga na kupata bao lililofungwa na Seleman Mwalimu lakini wakati mashabiki wao wakishangilia mwamuzi alipuliza filimbi kuashiria mfungaji aliotea.
Tukio hilo liliibua mzozo miongoni mwa wachezaji wa timu zote mbili na waamuzi kabla ya hali kutulia na mchezo kuendelea kama kawaida.
Wakizungumza baada ya mechi hiyo makocha wa timu hizo, Steve Barker wa Simba aliwasifia wachezaji wake licha ya kushindwa kupata ushindi wakati Pedro Concalves wa Yanga alisema mechi ilikuwa ngumu na kwamba Simba walitawala zaidi kipindi cha kwanza lakini wao Yanga walifanikiwa kuwadhibiti.
Mara ya mwisho Simba kutoka na ushindi mbele ya Yanga ilikuwa mwaka 2023 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, ushindi ambao ulipatikana kwa mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana.
Soka Yanga, Simba hakuna mbabe
Yanga, Simba hakuna mbabe
Read also
