Na mwandishi wetu
Matumaini waliyokuwa nayo Simba ya kucheza nusu fainali ya Kombe la
Shirikisho Afrika yametoweka baada ya timu hiyo kutolewa na Orlando
Pirates kwa mikwaju ya penalti.
Hiyo ni baada ya matokeo ya jumla ya bao 1-1. Simba ilishinda bao 1-0
mjini Dar es Salaam na Orlando nao kushinda bao 1-0 kwao Soweto,
Afrika Kusini.
Matokeo hayo yamehuzunisha wengi lakini Simba ilionesha ukomavu kwenye
michuano hiyo hasa kwa namna walivyopambana kwenye dakika 90 hizo za
mwisho za kufa au kupona.
Simba walijua fika kwamba wanacheza ugenini na timu ngumu, hivyo
walihitaji kutumia akili na mbinu za ziada ili kutafuta namna ya
kupenya nusu fainali kwa mara ya kwanza na kocha wa timu hiyo, Pablo
Franco alifanikiwa katika hilo kabla ya mambo kuanza kuharibika
baadaye.
Ukuta wa Berlin
Simba iliingia na mipango kabambe ya ulinzi madhubuti wanapokaba na
kushambulia kwa kasi kila walipopata nafasi hiyo. Simba walianza na
mabeki sita, viungo wa kati wawili, washambuliaji wawili huku
ikiwatumia mabeki wa kati watatu: Paschal Wawa, Joash Onyango na
Henock Inonga.
Mpango huo uliipa shida Orlando kupenya na kuiadhibu timu hiyo kwani
ilikaba kwa tahadhari na nidhamu na namna walivyokuwa wakigawana
kukaba kwa mawinga na katikati ya uwanja ilikuwa mtihani mkubwa kwa
Maharamia hao wa Baharini kupenya na kuleta madhara mpaka kipindi cha
kwanza kinamalizika.
Kadi ya Mugalu yatibua mambo
Uzito wa mechi uliendelea kutawala kwa Orlando licha ya kujaribu
kushambulia hapa na pale mpaka Chris Mugalu alipooneshwa kadi nyekundu
kwa kumchezea vibaya Olisa Ndah katika dakika ya 58.
Baada ya hapo, ilichukua dakika mbili kabla ya Innocent Maela kupiga
krosi iliyounganishwa kwa kichwa cha Kwame Peprah na kufanya mechi
ngumu kwa Simba ambao waliruhusu bao hilo wakiwa bado wana msongo juu
ya kadi ya Mugalu ambaye alikuwa akiwasumbua vilivyo mabeki wa
Orlando.
Sakho anyong’onyea
Pape Sakho aliyekuwa akicheza na Mugalu kwenye ushambuliaji alipunguza
makali kwa kuwa timu ilizidi kukaba na yeye akakosa msaada akiwa peke
yake mbele, safu nzima ya ulinzi ya Orlando ‘ikamuinamia’ kabla ya
baadaye kutolewa na kuingizwa Meddie Kagere.
Kwa kifupi Simba ilianza kuziba viraka wakati mechi ikiendelea na
kutoa mwanya kwa Orlando kuingiza washambuliaji wengi akiwemo
Gabadinho Mhango, mchezaji anayefahamika kwa kuwa na uwezo mkubwa.
Simba ilipambana
Pamoja na yote, Simba ilipambana kuzuia na kushambulia mara chache kwa
dakika takriban 30 zilizosalia kwa mipango ya Pablo na kufanikiwa
kutoruhusu bao jingine mpaka kipenga cha mwisho kinapulizwa na kuhamia
kwenye mikwaju ya penalti ambayo Simba hawakuwa na bahati nayo.
Ofori shujaa wa Orlando
Kipa wa Orlando, Richard Ofori alionesha ushujaa katika matuta hayo
ambapo kwanza alicheza penalti ya Jonas Mkude, penalti ya kwanza ya
Simba kabla ya baadaye kupewa penalti ya mwisho iliyokuwa ikiamua
hatma yao na kuukwamisha mpira wavuni na kuimaliza rasmi safari ya
Simba kimataifa.
Inonga ageuka gumzo
Ukiachana na matokeo hayo, ishu ya Inonga kutetemeka mwili huku
akionesha kuwa na wasiwasi mno baada ya kukosa penalti imeibua gumzo
kubwa na hali ya huzuni kwa waliokuwa wakifuatilia mchezo huo.
Inonga ambaye alionesha uimara usiotetereka kwa dakika zote 90 za
matumaini na huzuni za mechi hiyo alikosa penalti ya tatu ambayo
aliipiga kiufundi ‘akimuuza’ kipa lakini mpira ulizidi kipimo,
ukagonga mwamba wa juu na kwenda nje.
Hali hiyo ilionekana kumtesa mno Inonga kwani baadaye alioneshwa akiwa
amechuchumaa peke yake wakati penalti zikiendelea, alikuwa aking’ata
vidole, akitetemeka na kuonesha wasiwasi mkubwa mno. Baada ya hapo
wengi walimfariji na kumsikitikia kwa hali aliyokuwa akikutana nayo
kichwani mwake wakati huo.
Orlando dhidi ya Al Ahli
Orlando sasa itakutana na Al Ahli Tripoli ya Libya kwenye mchezo wa
nusu fainali. Al Ahli imetinga hatua hiyo baada ya kuichapa Al Ittihad
ya Libya pia kwa bao 1-0 kwenye ushindi wa jumla.
Nusu fainali nyingine itazikutanisha RS Berkane dhidi ya TP Mazembe
ambapo mechi za hatua hiyo zitapigwa Mei 8 kabla ya mechi za marudiano
Mei 15, mwaka huu.