Na mwandishi wetu
Baada ya Simba kuambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo, beki wa
timu hiyo, Shomari Kapombe amekiri kuwa presha ni kubwa kwao katika
kuelekea kusaka taji la Ligi Kuu ya NBC Bara.
Hii ni mechi ya tatu mfululizo, Simba inaambulia matokeo ya sare na
hivyo kuambulia pointi moja tu kwa kila mechi hali inayozidi kuifanya
ijiweke pagumu katika mbio za kusaka taji la ligi hiyo, kabla ya mechi
hiyo na Namungo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Mkapa, Simba ilipata
matokeo ya aina hiyo dhidi ya Yanga na Polisi Tanzania.
Kapombe aliyefunga bao la kwanza la Simba katika mchezo huo alisema
mchezo ulikuwa mgumu lakini walipambana kuhakikisha wanarejea kwenye
mstari wao na mwisho wakashuhudia sare hiyo ambayo inaongeza presha
kwao kwani wanahitaji matokeo kulingana na ushindani uliopo sasa
kuelekea mwisho wa ligi.
“Ni kweli presha ni kubwa kutokana na matokeo yenyewe lakini
tunafahamu kwamba tunahitaji ushindi na tunapambana kuhakikisha
tunaweka sawa haya matokeo, kama wachezaji tunahitaji kupambana
kuhakikisha tunamaliza kwa ushindi kwenye mechi zilizobaki kisha
tutaona tumemaliza kwenye nafasi gani,” alisema Kapombe.
Simba inashikilia nafasi ya pili ikiwa na pointi 43 ikijaribu kutetea
ubingwa wake dhidi ya Yanga iliyoko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu
ya NBC kwa pointi 55.
Licha ya sare hiyo kuendelea kuvuruga hesabu za Simba lakini pia
imevunja rekodi ya timu hiyo msimu huu ya kutoruhusu mabao mawili
kwenye mechi moja. Kuhusiana na hilo Kapombe amekiri ni makosa ambayo
hata benchi la ufundi limeyaona na itayafanyia kazi kuhakikisha
wanaendeleza ubora wao katika safu ya ulinzi.
Pamoja na hayo, Simba imefanikiwa kulinda vyema lango lake msimu huu
ikiwa na ‘clean sheet’ 12 ikizidiwa na Yanga pekee yenye clean sheet
- Simba pia ni ya pili kwa kuruhusu mabao machache msimu huu ikiwa
imefungwa mabao tisa nyuma ya Yanga iliyoruhusu mabao sita mpaka sasa.
