Na mwandishi wetu
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, John Bayo (pichani) amefariki Dunia Jijini Arusha leo Jumanne.
Mtoto wa marehemu aitwaye, Gilbert Bayo, alisema kwamba baba yake alianza kusumbuliwa na figo tangu Novemba, mwaka jana ambapo alifanyiwa upasuaji kwa kutolewa moja na hapo ndipo afya yake ilipoanza kudhoofika.
“Baba alikuwa akisumbuliwa na figo na mwaka jana alifanyiwa upasuaji akarudi nyumbani. Lakini baadaye alianza kuumwa tena na mwezi mmoja uliopita tukamleta Hospitali ya Ocean Road hadi Alhamisi ya wiki iliyopita alirudi huku Arusha na leo amefariki katika Hospitali ya Mount Meru,” alisema.
Alisema msiba upo nyumbani kwa John Bayo, Majengo mkoani Arusha ambapo taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika.
Katibu wa Kamisheni ya Wanariadha Tanzania, Andrew Robhi alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kiongozi huyo wa zamani.
“Watu wa riadha wamesikitishwa na tukio hili, nadhani taratibu za maazishi na wapi yatafanyika tutawatangazia. Kwa sasa mwili upo Mount Meru na msiba upo nyumbani kwake Majengo Arusha,” alisema kiongozi huyo.
“Huyu Mzee alikuwa muongozaji wa mbio mbalimbali zikiwemo Kilimanjaro Marathon na nyingine na ndiye aliyekuwa mpima njia maarufu, alikuwa mtu aliyeleta mabadiliko mengi na kufanya mengi. Sisi kama wanamichezo tutamkumbuka kwa mambo aliyofanya kwa ajili ya taifa letu,” alisema.
Licha ya Bayo kuwa ndiye msimamizi wa kambi ya Olimpiki mwaka jana, pia alikuwa wa kwanza kupeleka wanariadha Ulaya kuanzia miaka ya 1980 na ameendelea kuwa nguzo kuu katika uongozi wa riadha hadi mwisho wa uhai wake.
Riadha Bayo afariki dunia
Bayo afariki dunia
Read also