Na mwandishi wetu
Simba leo Jumamosi imetoka sare ya bila kufungana na Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mechi ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa mjini Francistown, Botswana.
Hiyo inakuwa sare ya pili kwa Simba baada ya sare ya bao 1-1 na Asec Memosas ya Ivory Coast katika mechi yake ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi mbili katika mechi mbili wakati Galaxy wanakuwa wamefikisha pointi nne na kuendelea kujiimarisha kileleni katika kundi hilo wakisubiri matokeo ya mechi kati ya Asec na Waydad Casablanca leo saa nne usiku.
Simba hata hivyo itabidi ijilaumu kwa kutoka sare mechi yake na Galaxy baada ya kuutawala mchezo kwa vipindi vyote viwili ikifanya mashambulizi ya mara kwa mara ambayo hayakuzaa matunda.
Dakika ya 24, Jean Baleke aliinasa pasi ya Shomary Kapombe na kusogea na mpira kabla ya kufumua shuti ambalo kipa wa Galaxy aliudaka mpira ambao ulimponyoka na kuelekea wavuni lakini akauwahi kabla haujavuka mstari.
Qalaxy waliibuka kidogo dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili na kulisogela lango la Simba ambapo katika jitihada za kuokoa, Henock Inonga alimchezea rafu mchezaji wa Galaxy na mwamuzi kuamuru upigwe mpira wa adhabu nje ya kidogo ya eneo la penalti.
Mpira huo wa adhabu ulionekana kuibua hofu kwenye lango la Simba lakini mpigaji alipaisha na kumfanya kipa Ayoub Larked wa Simba akiuangalia mpira huo kwa macho ukitoka nje ya lango.
Katika dakika ya 62, kocha wa Simba Abdulhaki Benchikha aliwatoa Willy Onana na kumuingiza Clatous Chama na Kanoute ambaye nafasi yake aliingia Muzamir Yassin.
Mabadiliko hayo yalizidi kuiongezea uhai Simba na kuzidi kulisogelea lango la Galaxy ambalo mabeki wake walikuwa na kazi ya kuokoa mashambulizi huku Simba wakikosa umakini katika umaliziaji.
Benchikha kwa mara nyingine katika dakika ya 77 aliwatoa Denis Kibu na nafasi yake kuingia Luis Miquissone na Saido Ntibazonkiza ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Moses Phiri.
Kwa mara nyingine Simba ilizidi kupata nguvu na dakika ya 84, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ alimpasia mpira Baleke ambaye aliingia nao vizuri ndani ya 18 lakini alionekana kama kujichanganya katika kuchukua maamuzi sahihi kabla ya kupiga pasi ya juu pembeni ambayo haikumfikia mchezaji yoyote wa Simba na mpira kutoka nje.
Katika dakika nne za nyongeza kabla ya mpira kumalizika, Chama akiwa katika utulivu aliunasa mpira na kupiga shuti lililogonga mwamba na mpira kurudi uwanjani kabla ya kumkuta Baleke ambaye alipiga shuti kubwa lililopaa juu na kutoka nje ya uwanja.
Katika dakika hizo hizo, Zimbwe Jr ambaye alikuwa nahodha wa Simba, aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Israel Mwenda, mabadiliko ambayo hayakubadili chochote.
Kimataifa Simba, Galaxy hakuna mbabe
Simba, Galaxy hakuna mbabe
Read also