Na mwandishi wetu
Hatimaye kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Adel Amrouche amewaita kikosini wachezaji wa Simba, beki wa kulia Shomari Kapombe na beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’.
Taarifa za kujumuishwa kwa mabeki hao zimeelezwa leo Jumapili na Rais wa TFF, Wallace Karia alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Amesema uteuzi huo umefanyika baada ya Stars kurejea nchini leo alfajiri baada ya kuumana na Uganda nchini Misri na kupata ushindi wa bao 1-0 ikiwa ni mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Africa (Afcon) 2023.
“Baada ya mwalimu (Adel) kurudi amewaita timu ya taifa, mabeki wetu wazoefu Shomari Kapombe na Mohamed Hussein, kwa hiyo nadhani wako kambini sasa hivi pamoja na timu.
“Kulikua na maneno mengi labda pengine mwalimu… Mwenyewe (Adel) ndiyo aliyechagua ile timu alipokuja alipewa orodha ya wachezaji, lakini mimi na Katibu (Said Yakubu, Katibu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo) tumekuwa na yule mwalimu na mazungumo nyuma miezi miwili kwa hiyo alikuwa anashiriki kuangalia ligi,” alisema Karia.
“Wakati huo tulikuwa tunaangalia namna gani tutamlipa mshahara, kwa hiyo hakushtukizwa, timu ile ya kwake alipewa na alikuwa anaifuatilia, si kwamba ametangazwa juzi tu ameita timu ya taifa, hapana timu ile ni ya kwake na amekuwa akiifuatilia zaidi ya miezi miwili,” alisema Karia.
Awali, Kapombe na Zimbwe Jr hawakujumuishwa kwenye kikosi hicho na kuibua sintofahamu kutokana na na ubora waliokuwa nao wachezaji hao ambao awali hawakujumuishwa kikosini.
Hata hivyo, wiki iliyopita Simba ilipoiadhibu Horoya AC mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Mkapa na Wekundu hao kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, mwisho wa mchezo huo, Amrouche alionekana akizungumza pembeni na mabeki hao na kuibua minong’ono ya pengine wataongezwa kikosini.
Stars inajiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Uganda utakaopigwa keshokutwa Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa, ikihitaji ushindi kujiweka kwenye mazingira mazuri.
Timu hiyo ipoa kwenye Kundi F, Stars ikishikilia nafasi ya pili na pointi zake nne, nyuma ya kinara Algeria mwenye pointi tisa wakati Niger ni ya tatu kwa pointi mbili na Uganda inaburuza mkia ikiwa na pointi moja.
