Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Tanzania, George Mpole anayekipiga FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ameahidi kuonesha kiwango bora katika timu yake mpya na kuisaidia kufanya vizuri.
Mpole ambaye ndiyo mara ya kwanza kucheza ligi nchini humo alijiunga na klabu hiyo hivi karibuni akitokea Geita Gold FC.
Akizungumzia makazi yake hayo mapya, Mpole alisema anashukuru kwa kuwa amepokewa vizuri hivyo hatowaangusha mashabiki na wale waliomuamini katika klabu hiyo.
“Namshukuru Mungu nimefika salama na kupokelewa vizuri kwa upendo, naahidi kuonesha nilichonacho kutoka Tanzania kuisaidia timu katika malengo yake,”alisema Mpole.
Mpole pia aliomba sapoti ya mashabiki wake wapya wa klabu hiyo akisema ni mara yake ya kwanza kucheza huko hivyo pale atakapopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza atafanya kile ambacho kilimpeleka huko huku akitegemea kuungwa mkono na wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
Mchezaji huyo aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu NBC msimu uliopita baada ya kufunga mabao 17 na kumshinda aliyekuwa mpinzani wake, Fiston Mayele wa Yanga aliyefunga mabao 16.
Ubora wake ulifanya baadhi ya klabu kadhaa nchini zikiwemo Simba, Yanga na Azam kutajwa kumuhitaji ingawa baadaye aliamua kutimkia kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
