Rabat Morocco.
Sadio Mane alimbwaga nyota mwenzake wa zamani wa Liverpool, Mohamed Salah katika fainali za Afcon 2021, swali lililopo sasa ni je nani kati yao jioni ya leo atatwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Afrika? Na vipi kuhusu Pape Ousmane Sakho wa Simba anayewania tuzo ya bao bora?
Mane na Salah watapambanishwa jioni hii katika hafla ya utoaji tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zitakazofanyika katika jiji la Rabat nchini Morocco huku wakiwa wamewaachia mashabiki wa soka Afrika na duniani kitendawili cha nani kumpiku mwenzake.
Baada ya kuwa pamoja Liverpool na kutoa mchango mkubwa kwenye mafanikio ya timu hiyo miaka ya hivi karibuni, Mane ametimkia Ujerumani na kujiunga na klabu ya Bayern Munich na kumuacha Salah akiendelea kukipiga Liverpool.
Hafla ya utoaji tuzo hiyo itawakutanisha wanamichezo mbalimbali wanaowania tuzo hizo katika vipengele tofauti tofauti huku kukiwa na mahudhurio ya watu mbalimbali maarufu wakiwamo viongozi wa soka na wachezaji magwiji wa zamani.
Habari kubwa ni kwa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka kwa upande wa wanaume ambapo mbali na Salah na Mane, mwingine ni kipa Edouard Mendy ambaye pia anaidakia Chelsea na kama Mane naye anatokea nchini Senegal ingawa wanaozungumzwa zaidi ni Mane na Salah.
Salah ambaye amewahi kutwaa tuzo hiyo, anajivunia mafanikio yake akiwa na Liverpool kwa kuibuka mfungaji bora na kutangazwa kuwa mchezaji bora profesheno wa mwaka wakati Mendy na Mane wao mbali na kuisaidia Senegal kuibuka kinara Afcon 2021 pia wameiwezesha timu hiyo kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Mchuano mwingine pia utakuwa kwenye soka la wanawake, Asisat Oshoala wa Nigeria atachuana na Mnigeria mwenzake, Perpetua Nkwocha pamoja na nahodha wa Cameroon, Ajara Nchout Njoya na Grace Chanda wa Zambia.
Kwa upande wa makocha wanawake, mpambano utakuwa kati ya kocha wa Mamelodi Sundowns Ladies, Jerry Tshabalala ambaye ana rekodi ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake atachuana na Bruce Mwape wa Zambia aliyeiwezesha timu yake kuiwakilisha Afrika kwenye Michezo ya Olimpiki 2020 na kufuzu faianli za Kombe la Dunia kwa Wanawake.
Wengine katika kundi hilo ni Desiree Ellis wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini, Banyana Banyana pamoja na Atlas Lionesses ambaye ni kocha wa timu ya wanawake ya Morocco ya Atlas Lionesses ambaye ameiwezesha timu yake kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Makocha wanaume mchuano ni kati ya kocha wa Senegal, Aliou Cisse aliyeiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Afcon pamoja na kufuzu Kombe la Dunia akiibwaga Misri iliyokuwa chini ya kocha mzoefu, Carlos Queiroz ambao pia watachuana na Walid Regragui, huyu ni kocha wa timu ya Waydad ya Morocco ambayo ameiwezesha kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa Watanzania hasa mashabiki wa Simba mbali na Salah na Mane, macho na masikio yao yatapenda kusikia na kumuona Pape Ousmane Sakho akitangazwa mshindi wa tuzo ya bao bora. Pape anawania tuzo ya bao bora akichuana na Gabadinho Mhango wa Malawi, Sakho anabebwa kwa bao la ‘tik taka’ alilofunga katika mechi ya Simba na ASEC Mimosas ya Ivory Coast wakati Mhango anabebwa na bao alilofunga katika mechi ya Afcon dhidi ya Morocco.
Hafla ya tuzo hizo itapambwa na wanamuziki maarufu Afrika akiwamo Tiwa Savage wa Nigeria, Asmaa Lamnawar wa Morocco pamoja na wasanii wa kundi la Magic System la Ivory Coast na kurushwa moja kwa moja kupitia vituo mbalimbali vya televisheni na kushuhudiwa katika nchi zaidi ya 40.
Kimataifa Mane, Salah nani kubeba tuzo CAF?
Mane, Salah nani kubeba tuzo CAF?
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
