Liverpool, England
Ushindi wa mabao 5-2 walioupata Real Madrid mbele ya Liverpool Jumanne usiku umewapa matumaini mapya na sasa wanadai kulitaka tena taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kulibeba msimu uliopita.
Kauli hiyo imetolewa na mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Karim Benzema ambaye katika mechi hiyo alifunga mabao mawili, Benzema alisifia kiwango chao na kisha kusema wanalitaka tena taji hilo.
“Tulicheza vizuri, tulitengeneza mabao na sasa tunalitaka taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara nyingine,” alisema Benzema.
“Baada ya dakika 15 tulianza kuiona Real Madrid ya ukweli, soka katika hatua hii unakuwa mchezo mgumu, walianza vizuri kuliko sisi lakini hii ni mechi kubwa na tulikuwa tayari kwa hilo,” alisema Benzema.
Kwa mabao mawili aliyofunga katika mechi hiyo ya hatua ya 16 bora ya ligi hiyo, Benzema katika hatua hiyo anakuwa wa tatu akiwa na mabao 31, nyuma ya Cristiano Ronaldo (mabao 67) na Lionel Messi (mabao 49).
Katika mechi hiyo dakika 15 za mwanzo zilikuwa ngumu mno kwa Real Madrid iliyokuwa ugenini baada ya kufungwa bao dakika ya nne ya mchezo mfungaji akiwa Nunez na dakika 10 baadaye Mohamed Salah akaongeza bao la pili kwa Liverpool.
Ubora na hadhi ya Real ilianza kuonekana dakika ya 20 baada ya Vinicius Junior kuifungia timu hiyo bao la kwanza kabla ya kusawazisha dakika 15 baadaye, mabao yaliyoibua matumaini mapya kwa Real.
Dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili, Liverpool walijikuta wakiumizwa kwa mara nyingine na Militao kabla ya mkongwe Benzema kukamilisha karamu ya mabao katika dakika za 55 na 66.
Iwapo Real watafanikiwa kulitwaa taji hilo kwa mara nyingine msimu huu, watakuwa wamefanya hivyo mara 15 katika historia ya ligi hiyo kubwa ya klabu barani Ulaya.