Roma, Italia
Majanga yameendelea kumuandama kocha wa Roma, Jose Mourinho ambaye amefungiwa siku 10 kwa kudai kuwa Daniele Chiffi ni mwamuzi wa hovyo aliyewahi kukutana naye katika maisha yake.
Mourinho ambaye hivi karibuni alifungiwa mechi nne za Uefa kwa kumbughudhi na kumtolea lugha kali mwamuzi Anthony Taylor, anadaiwa kutoa kauli dhidi ya Chiffi Mei 3 mwaka huu katika mechi kati ya Roma na Monza.
Sambamba na adhabu hiyo aliyopewa na Chama cha Soka Italia au FA, Mourinho kocha wa zamani wa timu za FC Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Man United na Tottenham, pia ametozwa faini ya Pauni 43,000
Kwa mujibu wa FA, Mourinho ataanza kuhesabiwa siku hizo 10 kuanzia siku ya kwanza ya msimu wa mashindano husika.
Katika mechi iliyomuingiza kwenye matatizo, Mourinho alikerwa na uamuzi wa Chiffi kumtoa kwa kumpa kadi nyekundu mchezaji wa Roma, Mehmet Zeki Celik katika dakika sita za nyongeza za mechi ya Serie A baina ya timu hizo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 huku Mourinho akipewa kadi ya njano katika mechi hiyo baada ya kutofautiana na mwamuzi huyo.
Msimu uliopita umekuwa mgumu kwa Mourinho ambaye hadi unamalizika alipewa kadi nyekundu mara tatu kutokana na kugombana na waamuzi, moja kati ya hizo alipewa na Chiffi Septemba mwaka jana katika mechi dhidi ya Atalanta, mechi ambayo Roma ilipoteza.
Roma imemaliza Serie A msimu uliopita ikiwa nafasi ya sita ingawa ilifikia hatua ya fainali ya Europa Ligi na kupoteza kwa penalti mbele ya Sevilla.
Kimataifa Mourinho afungiwa siku 10
Mourinho afungiwa siku 10
Read also