London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekataa kuitupia lawama teknolojia ya VAR baada ya timu yake kufungwa mabao 2-0 na West Ham badala yake amesema kwamba timu yake ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England (EPL) iliyopigwa jana Alhamisi, West Ham ilipata bao la kwanza dakika ya 13, bao lililozua mjadala na kulazimika kutumia teknolojia ya VAR kwa kilichoonekana kuwa mpira huo uliokolewa.
Bao hilo liliwakumbusha mashabiki bao pekee la ushindi la Newcastle katika mechi dhidi ya Arsenal iliyopigwa Septemba mwaka huu, bao ambalo nalo lilizua utata kiasi cha Arteta kulaumu matumizi ya VAR na kudai kuwa bao hilo ni aibu na fedheha katika EPL.
West Ham iliandika bao lake la pili dakika ya 55 lililofungwa na Konstantinos Mavropanos, matokeo ambayo yameinyima Arsenal nafasi ya kumaliza mechi 19 za mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni. Akizungumzia bao la West Ham Arteta alisema ni aibu kwamba pamoja na uwapo wa teknolojia bado kunakuwa na mjadala wa kama bao liliingia au halikuingia lakini mwisho wa siku hawana la kufanya.
Arsenal ilipiga mashuti 30 kwenye lango la West Ham na kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la wapinzani wao lakini hayo yote hayakuweza kuwasaidia kupata ushindi.
“Kama hatukufunga bao katika mashuti 30 maana yake ni kwamba tunatakiwa kujaribu kupiga mashuti 50 au 60 ili kufunga goli, hilo ndilo jambo pekee la kufanya,” alisema Arteta.
Kwa upande wake kocha wa West Ham, David Moyes alielezea furaha yake baada ya ushindi huo na kusema kwamba hivi karibuni atakaa na mabosi wake kujadili mpango wa kusaini mkataba mpya wakati mkataba wake wa sasa unafikia mwisho baada ya msimu huu.