Na mwandishi wetu
Uongozi Yanga umefariji mshambuliaji wao Fiston Mayele kuwa hata ikikikosa kiatu cha ufungaji bora msimu huu, asisikitike kwani aliyoyafanya msimu huu yanatosha kutambulisha ushujaa wake.
Hayo yamekuja ikiwa kesho kunatarajiwa kuchezwa mechi za mwisho za Ligi Kuu msimu huu huku Mayele akiwa amefungana kwa mabao 16 kileleni na mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole.
Wawili hao wamekuwa wakifukuzana kwa muda mrefu tangu kuanza kwa ligi na kesho wanatarajia kutegua kitendawili hicho wakati Yanga ikiumana na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Geita ikiwa ugenini dhidi ya Coastal Union.
“Lengo letu kwa Mayele limetimia la kutuwezesha kutwaa ubingwa, kwa hiyo imebaki malengo yake binafsi kama alivyosema na sisi tunamsapoti, tunampa asilimia 100 kuhakikisha anatimiza ndoto yake kwa kufunga mabao mchezo unaokuja ili atwae kiatu cha dhahabu,” alisema Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli.
“Ikitokea bahati mbaya Mayele asikate tamaa, yeye ni mshambuliaji bora sana, msimu uliopita akiwa Congo (AS Vita Club) alifunga mabao 13, msimu huu ameongeza matatu zaidi mpaka sasa kwa hiyo yeye ni mshambuliaji bora mpaka sasa kwa Tanzania pia, ameweka rekodi ya tofauti.
“Kwa sasa watu wote wanatetema, ana vitu vingi vikubwa vya kujivunia kuliko kiatu cha dhahabu ambacho tunatamani akipate lakini ikitokea kakosa bado ana mengi makubwa ya kujivunia msimu huu kwa Yanga na Tanzania, lakini tunamwombea afunge magoli awe mfungaji bora,” alisema Bumbuli.
Mechi nyingine za kesho ni kama ifuatavyo…
Azam v Biashara United
Dodoma Jiji v KMC
Kagera Sugar v Polisi Tanzania
Mbeya City v Namungo
Simba v Mbeya Kwanza
Ruvu Shooting v Tanzania Prisons.
